Rwanda yakanusha kuwatia mbaroni raia kinyume cha sheria na kuwatesa watuhumiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35525-rwanda_yakanusha_kuwatia_mbaroni_raia_kinyume_cha_sheria_na_kuwatesa_watuhumiwa
Serikali ya Rwanda leo imekanusha madai ya Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch na kusema kuwa, madai hayo hanayana msingi wowote
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Oct 11, 2017 13:16 UTC
  • Rwanda yakanusha kuwatia mbaroni raia kinyume cha sheria na kuwatesa watuhumiwa

Serikali ya Rwanda leo imekanusha madai ya Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch na kusema kuwa, madai hayo hanayana msingi wowote

Kabla ya hapo shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti yake inayolituhumu jeshi la Rwanda kwamba, limekuwa likiwatia mbaroni raia kinyume cha sheria na kuwatesa vibaya.

Ripoti hiyo ya Human Rights Watch imeeleza kwamba, jeshi la Rwanda limekuwa likiwatesa vibaya watuhumiwa liliowatia mbaroni kinyume cha sheria na kuwalazimisha wakiri makosa ambayo hawakuyafanya. Ripoti hiyo imeashiria visa 104 vya kutiwa mbaroni kinyume cha sheria raia kunakofanywa na jeshi la Rwanda.

Ripoti hiyo ambayo imeandaliwa baina ya mwaka 2010 na 2016 inaelerza kuwa, wengi kati ya waliotiwa mbaroni kinyume cha sheria na jeshi la Rwanda waliteswa vibaya kwa kupigwa shoti kwa nyaya za umeme hukuu baadhi yao wakinyongwa bila hata ya kufunguliwa mashtaka.

Diane Shima Rwigara, mpinzani wa Rais Kagame ambaye kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea uasi

Ida Sawyer, Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika ukanda wa Afrika ya Kati anasema kuwa,  uchunguzi wa miaka kadhaa iliyopita unaonyesha kwamba,  maafisa wa kijeshi wa Rwanda wamekuwa wakitumia mateso kama wenzo wao wa kupata taarifa kutoka kwa watuhumiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch aghalabu ya raia hao wanatiwa mbaroni kwa sababu tu ya kushukiwa kwamba, ni wanachama wa kundi la waasi la FDLR linaloendesha harakati zake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Rais Paul Kagame wa Rwanda anasifiwa kimataifa kwa kurejesha amani nchini Rwanda na kustawisha uchumi wa nchi hiyo haraka baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994. Hata hivyo kiongozi huyo analaumiwa na jumuiya za kutetea haki za binadamu kwamba, anabana uhuru wa vyombo vinavyojitegemea vya habari na kukandamiza wapinzani wake.