Umoja wa Afrika waunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesisitiza kuwa, umoja huo unaunga mkono kikamilifu makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Moussa Faki ametangaza katika taarifa yake kwamba, umoja huo kama zilivyo asasi nyingine za kimataifa umepokea kwa mikono miwili makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na unaamini kwamba, ushindi wa kidiplomasia wa pande kadhaa na uliokuwa na athari umethibitisha kwamba, mazungumzo nio mbinu na njia mwafaka ya kuzipatia ufumbuzi hitilafu na mivutano.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ameeleza kuwa, kulindwa na kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na pande husika katika makubaliano hayo ni jambo la dharura hasa kwa kutilia maanani kwamba, makubaliano hayo yamethibitishwa na kuungwa mkono Wakkala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
Moussa Faki ameashiria nafasi muhimu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA katika uthabiti wa Mashariki ya Kati na kusisitiza udharura wa kutumia utendaji wa pande kadhaa kama mbinu ya uhakika na athirifu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kimataifa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, serikali ya Marekani imeendelea kukosolewa kila kona ya dunia kutokana na hatua yake ya kukwamisha utekelezwaji wa makubaliano hayo ya nyuklia na kuendelea kuituhumu Iran kwamba, haijafungamana na makubaliano hayo. Hii ni katika hali ambayo ripoti zote za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA zinaonyesha kwamba, hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba, Iran imekiuka makubaliano hayo.