Uungaji mkono wa Umoja wa Afrika kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesisitiza kuwa, umoja huo unaunga mkono kikamilifu makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Moussa Faki Mahamat, amesisitiza katika taarifa yake kwamba, umoja huo kama zilivyo akthari ya asasi nyingine za kimataifa umepokea kwa mikono miwili makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na unaamini kwamba, hiyo ni ishara ya ushindi wa kidiplomasia wa pande kadhaa na uliokuwa na athari ambao umethibitisha kwamba, mazungumzo ni mbinu na njia mwafaka ya kuzipatia ufumbuzi hitilafu na mivutano ya kimataifa.
Uungaji mkono huo wa Umoja wa Afrika inafuatia matamshi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani. ambaye alisema siku ya Ijumaa kwamba, makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kwa kifupi, ndiyo makubaliano mabaya zaidi katika historia ya Marekani na akatishia kwamba, nchi yake itajitoa katika makubaliano hayo. Matamshi hayo ya Trump yamekabiliwa na radiamali hasi na pana kimataifa hususan nchi za Ulaya ambazo zimesisitiza juu ya udharura wa kuheshimiwa na kutekelezwa makubaliano hayo.
Katika uwanja huo, himaya ya Umoja wa Afrika kwa niaba ya nchi za bara la Afrika ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa katika pembe tofauti; kama ambavyo hatua hiyo inaonyesha kwa mara nyingine tena kutengwa siasa za Marekani ulimwenguni. Nchi za Kiafrika ambazo akthari yazo ni wahanga wa siasa za utumiaji mabavu na ungiliaji mambo wa Marekani na ulimwengu wa Magharibi, hivi sasa kwa kutangaza kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa mara nyingine tena zimesisitiza kwamba, utatuzi wa kidiplomasia ni njia mwafaka ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kimataifa.
Katika upande mwingine, kutokana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupigania uadilifu na kupinga dhulma, uonevu na ukandamizaji, daima imekuwa ikizingatiwa na akthari ya nchi za Kiafrika. Nyingi kati ya nchi za bara hilo zinaitambua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama mfano wa kuigwa uliofanikiwa katika nyuga mbalimbali. Ukuruba wa kidini wa Iran na nchi nyingi za Kiafrika, nayo ni sababu nyingine ya nchi hizo kuwa pamoja na Jamhuri ya Kiislamu. Hilo linashuhudiwa wazi katika mahusiano na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya pande mbili hizi katika nyuga mbalimbali likiwemo suala la ushirikiano na mahusiano ya kiuchumi.
Habibullah Ansari, Naibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Bara la Afrika lina wakazi bilioni moja na milioni 200 na nchi zote za Kiafrika zina mazingira mazuri kwa ajili ya kupanua na kustawisha uwekezaji katika nyanja za kibiashara, kiuchumi na nyuga nyingine.
Katika suala la makubaliano ya nyuklia ya JCPOA pia, nchi za Kiafrika zinaitambua Iran kama dola lenye nguvu, nchi ambayo kwa kung'ang'amia haki yake na kupitia njia ya mazungumzo imeweza kufikia makubaliano ambayo si tu kwamba, yana himaya ya kimataifa, bali imetoa kiigizo mwafaka kwa nchi nyingi za Kiafrika kwa ajili ya kufikia mafanikio na malengo yao katika kukabiliana na ubeberu.
Hatua ya Iran ya kutetea haki yake ya nishati ya nyuklia na kusisitiza kuheshimiwa bila ya ubaguzi Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia NPT ni jambo muhimu sana ambalo linazifungulia milango nchi za Kiafrika ya kujipatia teknolojia hiyo ya kisasa ya nishati ya nyuklia.
Katika hali ambayo, vita na machafuko ni mambo yanayoshuhudiwa yakiendelea katika nchi nyingi za Kiafrika na vita hivyo vimekuwa tishio kubwa kwa bara hilo, makubaliano ya nyuklia yameonyesha kuwa, njia ya mazungumzo inaweza kutumiwa kutatua hitilafu nyingi na kwa muktadha huo kuleta amani ya kudumu katika bara hilo.
Kuhusiana na jambo hilo, Alpha Conde, Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika anasema: Nchi za Kiafrika zina haja ya kutafuta njia na mikakati ya kuhitimisha mapigano na vita vya ndani kupitia njia ya mazungumzo na utatuzi wa amani na hivyo kunyamazisha milio ya risasi za bunduki.