UNICEF yatahadharisha kuhusu kuendelea ndoa za watoto wadogo barani Afrika
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limetahadharisha kuhusu madhara ya kuendelea kuozeshwa watoto wadogo barani Afrika.
Shirika hilo limetoa ushahidi kutoka katika ripoti iliyotolewa kwenye kikao cha wakuu wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa mjini Dakar Senegal na kusema kuwa, kuna ulazima wa kukabiliana vilivyo na ndoa za watoto wadogo katika maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika.
Ripoti hiyo imetolewa kwa lengo la kutafuta njia za kukabiliana na hatari zinazotokana na kuozeshwa wasichana wakiwa na umri mdogo barani Afrika. Ripoti hiyo imesema kuwa, suala la kupambana na mila na tabia hiyo linahitajia miaka mia kwani limejikita katika masuala ya kijamii na kiutamaduni kwenye eneo hilo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limeongeza kuwa, umaskini, usalama mdogo, mila na desturi pamoja na itikadi za jadi ndizo sababu kuu za kuozeshwa wasichana kabla ya kubaleghe katika maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika.
Nchi ambazo zimeathiriwa zaidi na tabia hiyo ni Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Mali, Burkina Faso na Guinea na ndizo nchi zenye idadi kubwa ya watoto wanaoozeshwa wakiwa na umri mdogo duniani.