Dunford: Marekani imeazimia kujiimarisha zaidi kijeshi barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35908-dunford_marekani_imeazimia_kujiimarisha_zaidi_kijeshi_barani_afrika
Mkuu wa Jeshi la Marekani amesema kuwa, nchi yake ina nia ya kujiimarisha kabisa kijeshi barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 24, 2017 04:03 UTC
  • Dunford: Marekani imeazimia kujiimarisha zaidi kijeshi barani Afrika

Mkuu wa Jeshi la Marekani amesema kuwa, nchi yake ina nia ya kujiimarisha kabisa kijeshi barani Afrika.

Jenerali Joseph Dunford ametangaza habari hiyo na kusema kuwa lengo la Marekani la kuongeza idadi ya wanajeshi wake barani Afrika ni kuwasaka na kuwatia mbaroni magaidi wa Daesh ambao baada ya kusambaratika khilafa yao huko Raqqah Syria na Mosul Iraq, wamekimbilia maeneo mengine duniani kujenga ngome zao mpya.

Mkuu huyo wa jeshi la  Marekani amegusia pia mapigano yaliyotokea tarehe 4 mwezi huu wa Oktoba nchini Niger na kupelekea wanajeshi wanne wa Marekani kuuawa na kusisitiza kuwa, magaidi wa Daesh bado ni tishio barani Afrika, kuanzia nchini Libya hadi katika rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri na kuanzia mashariki mwa Afrika hadi magharibi mwa bara hilo.

Nchi za Magharibi zimekuwa zikiingilia waziwazi masuala ya ndani ya nchi za Afrika

 

Itakumbukwa kuwa, viongozi mbalimbali wa Marekani akiwemo rais mwenyewe wa nchi hiyo, Donald Trump wamekiri mara kadhaa kwamba wao ndio waliounda magenge ya kigaidi kama vile Daesh. Mara kwa mara Marekani inatumia kisingizio cha kupambana na magaidi hao ili kufanikisha malengo yake ya kibeberu katika maeneo tofauti duniani.

Mkuu wa Jeshi la Marekani aidha amesema, karibuni hivi wizara ya ulinzi ya nchi hiyo Pentago itatoa mapendekezo yake kwa rais wa nchi hiyo Donald Trump na waziri wake wa ulinzi, James Mattis kuhusiana na udharura wa kuongezwa idadi ya wanajeshi wa Marekani barani Afrika kwa ajili ya kupambana na magaidi wa Daesh.

Hivi sasa kuna zaidi ya wanajeshi 1300 wa kikosi maalumu cha Marekani barani Afrika suala ambalo linalifanya bara la Afrika kuwa eneo lenye idadi kubwa zaidi ya wanajeshi wa kikosi maalumu cha Marekani baada ya Mashariki ya Kati.