Safari ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35920-safari_ya_balozi_wa_marekani_katika_umoja_wa_mataifa_barani_afrika
Nikki Haley, balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa anafanya safari barani Afrika akiwa mjumbe maalumu wa Rais Donald Trump anayeuongoza ujumbe wa nchi yake
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 24, 2017 11:44 UTC
  • Safari ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa barani Afrika

Nikki Haley, balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa anafanya safari barani Afrika akiwa mjumbe maalumu wa Rais Donald Trump anayeuongoza ujumbe wa nchi yake

Nikki Haley ametangaza kuwa, lengo la safari yake hiyo ni kubadilisha hali ya baadhi ya nchi za bara hilo na kupanua ushirikiano wa Marekani na nchi hizo. Katika safari hiyo ya kiduru, jana Jumatatu Nikki Haley aliwasili Addis Ababa  Ethiopia ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Baada ya Ethiopia, balozi huyo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa anatarajiwa kuelekea Juba na Kinshasa, miji mikuu ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa utaratibu. Mbali na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo, Nikki Haley atakutana pia na wasimamia amani wa Umoja wa Mataifa katika nchi hizo.

Baada ya mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Ethiopia na afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Afrika, Haley amesema kuwa, ana matumaini safari hiyo itafungua ukurasa mpya wa mahusiano imara na Umoja wa Afrika na washirika wa Kiafrika wa Washington. 

Nikki Haley, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa akifanya mazungumzo na  Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia

Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni nchi mbili barani Afrika ambazo zinakabiliwa na machafuko ambapo Washington inafanya juhudi za kuwashinikiza viongozi wa nchi hizo wafanye mazungumzo ili kuhitimisha migogoro ya kisiasa ya nchi zao. Hii ni katika hali ambayo, Marekani yenyewe ilikuwa miongoni mwa nchi zilizounga mkono kujitenga Sudan Kusini na Sudan. 

Safari ya Nikki Haley barani Afrika inafanyika kufuatia ahadi ya hivi karibuni ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa viongozi wa Afrika. Bara la Afrika daima limekuwa likikodolewa macho ya tamaa na madola makubwa kutokana na  utajiri mkubwa lilionao na nafasi yake muhimu ya kijiografia. Ndio maana katika duru mbalimbali, viongozi wa Marekani na madola ya Magharibi wamekuwa wakitekeleza siasa tofauti kwa bara hilo. Katika miongo ya hivi karibuni pia, bara la Afrika limekuwa likizingatiwa katika stratejia za kiuchumi na kisiasa za nchi za Russia na China na baadhi ya nchi za Kiarabu.

 

Rais Donald Trump wa Marekani

Pamoja na hayo, Rais Trump, si tu kwamba, hajachukua misimamo maalumu na ya wazi kuhusiana na nchi za bara la Afrika, bali amepunguza bajeti ya nchi yake kama ya kupambana na maradhi ya ukimwi barani Afrika na kuziweka baadhi ya nchi za bara hilo katika orodha ya nchi ambazo raia wake wamepigwa marufuku kufanya safari nchini Marekani, hatua ambazo zimezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa viongozi wa Kiafrika. 

Pamoja na kuwa, Rais Trump hajaonyesha wazi na rasmi shauku na mapenzi yake kwa bara la Afrika, lakini bara hilo lina umuhimu maalumu kwa Marekani hasa katika uga wa kiusalama, kiuchumi na kisiasa. Hivi sasa kuna wanajeshi wa Marekani katika nchi nyingi za Afrika ambao wamepelekwa huko kwa kisingizio cha kwenda kupambana na ugaidi na makundi yenye misimamo mikali.

Ripoti zinaonyesha kuwa, baada ya Mashariki ya Kati, Marekani ina vikosi vyake vingi maalumu barani Afrika. Takwimu zinaonyesha kuwa, Marekani ina kikosi maalumu cha askari 1300 barani Afrika.

Nikki Haley, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa

Kuuawa wanajeshi wanne wa Marekani huko nchini Niger hivi karibuni, ni ushahidi wa wazi wa kuweko wanajeshi wa nchi hiyo barani Afrika. Katika suala la biashara na uchumi pia, bara la Afrika linahesabiwa kuwa soko muhimu mno hasa kutokana na idadi kubwa ya watu na nguvukazi kijana.

Kwa kuzingatia ukweli huo, hata kama Rais Trump anasisitiza katika siasa zake za kiuchumi juu ya kuimarisha uchumi wa ndani ya Marekani, lakini uchumi wa nchi hiyo si tu kwamba, hauhitajii soko hilo la ndani, bali katika ushindani na nchi nyingine, bara la Afrika lina mvuto maalumu kwa nchi hiyo ya Magharibi.