Oct 29, 2017 15:59 UTC
  • Wakuu wa usalama wapigwa kalamu kufuatia mashambulizi ya kigaidi Somalia

Wakuu wa vyombo vya usalama nchini Somalia wamepigwa kalamu nyekundu kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya jana Jumamosi yaliyosababisha makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Shirika la habari la Reuters limenukuu ripoti iliyochapishwa na tovuti ya radio ya serikali ya Somalia inayosema kuwa: Baada ya kikao cha dharura cha baraza la mawaziri na wakuu wa usalama, Kamanda Mkuu wa Polisi, Jenerali Abdihakim Dahir Saiid na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Taifa ya Intelijensia na Usalama NISA, Abdullahi Mohamed Ali wamefutwa kazi.

Miongoni mwa shakhsia waliouawa katika mashambulizi hayo ya jana Jumamosi ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa jimbo la Kusini Magharibi, Madoobe Njunow Mohammed, Mbunge wa zamani Andinasir Garane na Kanali Yusuf Nur, afisa mwandamizi wa polisi ya federali ya Somalia.

Huku hayo yakirifiwa, idadi ya watu waliopoteza maisha katika mashambulio hayo imeongezeka na kufikia 29. Kadhalika watu 30 walijeruhiwa katika hujuma hizo, zilizolenga hoteli mashuhuri ya Nasa-Hablod katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu siku ya Jumamosi.

Shambulizi la wii mbili zilizopita, lililoua watu zaidi ya 300

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limedai kuhusika na hujuma hiyo. Taarifa zinasema magaidi waliwashikilia mateka watu kadhaa tokea jana usiku hadi leo asubuhi wakati maafisa wa polisi walipoingilia kati na kuwanushuru mateka hao. Maafisa wa usalama wanasema wamefanikiwa kuwakamata wakiwa hai magaidi watatu huku wengine wawili wakijilipua baada ya kufyatuliwa risasi.

Mashambulio ya jana Jumamosi yamejiri wiki mbili bada ya watu 350 kuuawa katika hujuma nyingine ya kigaidi mjini Mogadishu ambayo ilitajwa kuwa hujuma mbaya zaidi ya kigaidi kuwahi kushuhudiwa Somalia.

Tags