Majaji wa Mahakama ya Kilele ya Kenya wanyimwa ulinzi wa ziada
Serikali ya Kenya imekataa ombi lililowasilishwa na majaji wa Mahakama ya Kilele ya nchi hiyo wakitaka kupatiwa ulinzi wa ziada baada ya mmoja wa walinzi wao kupigwa risasi na hivyo kuwazuia kusikiliza kesi ililiyowasilishwa mahakamani na wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu ambayo ingepelekea kuakhirishwa uchaguzi wa marudio wa urais wa wiki iliyopita.
Mahakama ya Kilele ya Kenya ilitazamiwa kukutana tarehe 25 mwezi huu kusikiliza kesi hiyo iliyotaka kuakhirishwa uchaguzi wa marudio wa rais. Hata hivyo siku moja kabla ya kikao hicho mlinzi wa Philomena Mwilu, Naibu Jaji Mkuu alipigwa risasi na watu wasiojulikana.
Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga tarehe 25 mwezi huu alifika mahakamani, lakini idadi ya majaji watano haikutumia na ndipo Jaji Mkuu huyo aliposhindwa kutoa uamuzi kuhusu kesi hiyo na hivyo kutoa mwanya wa kufanyika uchaguzi huo wa marudio kama ilivyopangwa.
Mahakama ya Kilele ya Kenya ilitengua matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 8 mwaka huu nchini humo ikisema kuwa kuligunduliwa baadhi ya kasoro katika uchaguzi huo na kisha ikaagiza uchaguzi wa marudio ufanyike katika muda wa siku 60. Uamuzi huo ulikuwa wa kwanza wa aina yake kutolewa barani Afrika ambako kwa kawaida majaji wa mahakama huwa chini ya mashinikizo ya serikali zilizoko madarakani.
Uhuru Kenyatta ameshinda uchaguzi wa marudio wa urais wa Alhamisi iliyopita kwa kupata asilimia 98 ya kura baada ya Raila Odinga kiongozi wa muungano wa upinzani (Nasa) kususia uchaguzi huo. Raila alisema kuwa uchaguzi huo wa marudio usingekuwa huru na wa kiadilifu kwa sababu Tume ya Uchaguzi ya Kenya imeshindwa kutekeleza marekebisho aliyoyapendekeza baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kilele.