Eneo la Pwani latoa wito wa kujitenga na ardhi ya Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36149-eneo_la_pwani_latoa_wito_wa_kujitenga_na_ardhi_ya_kenya
Viongozi wa eneo la Pwani nchini Kenya wametoa mwito wa kutaka kujitenga eneo hilo na ardhi ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 03, 2017 23:50 UTC
  • Eneo la Pwani latoa wito wa kujitenga na ardhi ya Kenya

Viongozi wa eneo la Pwani nchini Kenya wametoa mwito wa kutaka kujitenga eneo hilo na ardhi ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Gavana wa kaunti ya Mombasa, Ali Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Jeffa Kingi waliongoza wabunge 12 wa Pwani ya Kenya katika kutoa mwito huo jana Ijumaa.

Gavana Joho amesema "Huu ndio mwanzo wa kutimiza ndoto ya Wapwani ya kutaka kujitenga na Kenya".

Amesema tayari timu ya mawakili wa ndani na nje ya nchi wameanzisha mazungumzo na mchakato wa kuhakikisha kuwa kanda ya Pwani inajitenga na Kenya.

Ramani ya Kenya

 

Gavana wa Kilifi kwa upande wake amesisitiza kuwa, katika safari yao hiyo ya kujitenga, watahakikisha kuwa hawatumii njia zisizo za kisheria na pia wataanza kupokea maoni ya wakazi wa eneo hilo kuhusu kadhia hiyo.

Jopo la wabunge wa Pwani ya Kenya limesema litawasilisha muswada katika Bunge la nchi hiyo, wa kutaka eneo hilo lipewe mamlaka ya kujitawala lenyewe.

Haijabainika iwapo hii ni moja ya mikakati ya mrengo wa upinzani wa NASA ulioapa kuanzisha uasi wa kiraia dhidi ya serikali, sambamba na kutaka wafuasi wao wasusie bidhaa na huduma za kampuni zinazoaminika kumilikiwa na viongozi wa chama tawala cha Jubilee, kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.