Marekani yakosolewa kwa kuzidi kujikita kijeshi barani Afrika
Kundi linalopinga vita liitwalo "Kituo cha Uchukuaji Hatua Kimataifa" limetangaza kuwa kuongezeka harakati na uwepo wa kijeshi wa Marekani katika bara la Afrika hakuna uhusiano wowote na mapambano dhidi ya ugaidi.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Russia Today kundi hilo linalopinga vita la Kituo cha Uchukuaji Hatua Kimataifa lenye makao yake nchini Marekani limetoa taarifa inayosisitiza kwamba stratijia ya kijeshi ya Washington barani Afrika haina uhusiano wowote na mapambano dhidi ya ugaidi.
Taarifa ya kundi hilo imebainisha kuwa Marekani imeongeza idadi ya wanajeshi wake katika bara la Afrika kwa ajili ya kudhamini manufaa na maslahi yake, kwa maana kwamba hatua ya jeshi la Marekani ya kutumia zaidi askari wa kikosi chake maalumu na kujichukulia hatua mkononi za kuua na kunyonga watu kila leo ni njama inayolenga kuzusha hali ya mchafukoge na kufanya uharibifu mkubwa katika kila pembe ya bara hilo.
Kundi linalopinga vita la Kituo cha Uchukuaji Hatua Kimataifa limeongeza kuwa kuna kila sababu ya kutokubaliana na visingizio vinavyotolewa kwamba Marekani inapambana na kundi la Daesh (ISIS) barani Afrika, kwa sababu Washington imeandaa mipango na mikakati ya kuunyonya utajiri wa nchi za Afrika na kuyadhibiti masoko ya kiuchumi ya bara hilo.
Katika muendelezo wa sera zake za kikoloni katika bara la Afrika na kwa kisingizio cha "utoaji mafunzo, uratibu wa majeshi ya nchi za Kiafrika na kushiriki katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi" Washington imeongeza mara tatu idadi ya askari wake barani humo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.../