Jeshi la Somalia lakomboa maeneo muhimu yaliyokuwa chini ya al-Shabaab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36187-jeshi_la_somalia_lakomboa_maeneo_muhimu_yaliyokuwa_chini_ya_al_shabaab
Vikosi vya jeshi la Somalia vimefanikiwa kukomboa ngome nyeti zilizokuwa chini ya makucha ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika maeneo ya Shabelle ya Chini na Kati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 05, 2017 11:36 UTC
  • Jeshi la Somalia lakomboa maeneo muhimu yaliyokuwa chini ya al-Shabaab

Vikosi vya jeshi la Somalia vimefanikiwa kukomboa ngome nyeti zilizokuwa chini ya makucha ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika maeneo ya Shabelle ya Chini na Kati.

Kamandi ya Jeshi la Taifa la Somalia SNA imetangaza leo Jumapili habari hizo na kuongeza kuwa, vijiji vilivyokombolewa toka mikononi mwa al-Shabaab katika maeneo hayo ni Basra, Bulo-Kuto, Daniga Balow, na Jabalul.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa sasa vikosi hivyo vya Somalia vinapambana na wapiganaji wa genge hilo lenye mafungamano na kundi la kitakfiri la Daesh (ISIS) ili kuwatimua kabisa katika ngome chache zilizosalia.

Habari hizo za kukombolewa maeneo hayo muhimu yaliyokuwa yakishikiliwa na al-Shabaab zimekuja chini ya masaa 48, baada ya Ethiopia kutuma maelfu ya askari katika nchi hiyo jirani, kusaidia katika jitihada za kieneo za kupambana na kundi la magaidi wakufurishaji wa al-Shabaab ambao wamekuwa wakitekeleza hujuma nchini humo na katika nchi jirani.

Wanajeshi wa Ethiopia wakiingia nchini Somalia

Mapema mwezi huu, kundi hilo la kigaidi liliuteka mji wa Rassadi ulioko kusini mwa Somalia baada ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika AMISOM kuondoka katika eneo hilo.

Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa Somalia ametangaza azma ya serikali yake ya kupambana na magaidi katika nchi hiyo ambayo wiki za hivi karibuni imepoteza mamia ya raia katika mashambulio ya al-Shabaab.