Miripuko minne ya mabomu yatokea katika eneo linalozungumza Kiingereza nchini Cameroon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36370-miripuko_minne_ya_mabomu_yatokea_katika_eneo_linalozungumza_kiingereza_nchini_cameroon
Maafisa wa Cameroon wametangaza habari ya kutokea miripuko minne katika eneo moja linalozungumza lugha ya Kiingereza nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 13, 2017 15:07 UTC
  • Wanajeshi wa Cameroon
    Wanajeshi wa Cameroon

Maafisa wa Cameroon wametangaza habari ya kutokea miripuko minne katika eneo moja linalozungumza lugha ya Kiingereza nchini humo.

Maafisa hao wamenukuliwa na shirika la habari la AFP wakisema leo kwamba, miripuko hiyo minne ilitokea jana usiku katika mji wa Bamenda unaozungumza Kiingereza. Hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyeuawa zaidi ya hasara za mali zilizosababishwa na miripuko hiyo.

Tangu mwezi Novemba 2016, maeneo yanayozungumza lugha ya Kiingereza yamekumbwa na mgogoro wa kijamii na kisiasa.

Machafuko katika moja ya miji inayozungumza Kiingereza nchini Cameroon

 

Karibu asilimia 20 ya jamii ya watu milioni 20 wa Cameroon wanazungumza Kiingereza. Wananchi hao wanaipinga serikali ya Rais Paul Biya na wanaamini kuwa imewatenga na kuyapuuza maeneo yao.

Mwezi Oktoba mwaka huu pia, maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini Cameroon yalikumbwa na machafuko. Iliripotiwa kuwa watu wasiopungua 17 waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa serikali na wengine wengi kujeruhiwa katika machafuko na maandamano ya wananchi hao wa Cameroon wanaotaka kujitenga maeneo yanayozungumza lugha ya Kiingereza.

Maandamano na machafuko ya mwezi Oktoba yalikuwa ni muendelezo wa machafuko ya kisiasa na kijamii yaliyoyakumba maeneo hayo  tangu mwezi Novemba mwaka jana.

Mbali na machafuko hayo, Cameroon inakabiliwa pia na mashambulizi ya mara kwa mara ya genge la kigaidi la Boko Haram.