Mahakama ya ICC yathibitisha mashtaka 70 dhidi ya kamanda wa LRA
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i3670-mahakama_ya_icc_yathibitisha_mashtaka_70_dhidi_ya_kamanda_wa_lra
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi imethibitisha mashtaka 70 yanayomkabili Dominic Ongwen, kamanda wa zamani wa kundi la waasi wa kaskazini mwa Uganda wa Lords Resistance Army (LRA).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 23, 2016 21:31 UTC
  • Mahakama ya ICC yathibitisha mashtaka 70 dhidi ya kamanda wa LRA

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi imethibitisha mashtaka 70 yanayomkabili Dominic Ongwen, kamanda wa zamani wa kundi la waasi wa kaskazini mwa Uganda wa Lords Resistance Army (LRA).

Mahakama hiyo imesema kuwa, miongoni mwa mashtaka yanayomkabili Ongwen ni uhalifu wa kivita, ubakaji, mauaji ya halaiki na kuwatumia wanawake katika utumwa wa ngono. Dominic Ongwen, alikamatwa yapata mwaka mmoja uliopita huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na kukabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Ongwen anakuwa kamanda wa kwanza wa LRA kupandishwa kizimbani katika mahakama ya ICC akikabiliwa na mashtaka ya jinai dhidi ya binadamu. Dominic Ongwen ni miongoni mwa makamanda watano wa ngazi za juu wa kundi la waasi wa LRA waliokuwa wakisakwa na mahakama ya ICC kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu. Kundi hilo la waasi lilianzisha harakati zake nchini Uganda na baadaye likapanua wigo wa harakati hizo hadi katika nchi za Sudan Kusini, Chad na hata katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa kundi la waasi wa Uganda la Lord's Resistance Army (LRA) limeua zaidi ya watu laki moja na kuteka nyara watoto elfu sitini ambao baadhi yao wanatumiwa kama watumwa wa ngono.