Sudan katika jitihada za kustawisha uhusiano wake na Russia
Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan ambaye alikuwa safarini mjini Moscow ameitaka Russia kuilinda Khartoum mbele ya uingiliaji kati wa Marekani nchini Sudan.
Al Bashir ameashiria kwamba, masuala mengi yanayolikabili eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ya Afrika yanatokana na uingiliaji kati wa Marekani na kusisitiza kuwa, kugawanywa Sudan katika sehemu mbili pia ni matokeo ya siasa za serikali ya Washington. Rais wa Sudan ameongeza kuwa, nchi yake inahitajia ulinzi mbele ya siasa na hatua za kiuhasama za Marekani.
Safari ya Omar al Bashir nchini Russia ni ya kwanza kufanywa na Rais wa Sudan nchini humo baada ya kupita miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili. Al Bashir ambaye katika miaka ya hivi karibuni amefanikiwa kuchota kitita kikubwa cha fedha kutokana na kujikurubisha kwa Saudi Arabia, sasa anataka kupanua zaidi uhusiao wa nchi yake na nchi nyingine hususan Russia. Katika miezi kadhaa iliyopita pia al Bashir alifanya mashauriano mapana na maafisa wa serikali ya Washington na baadaye Sudan imeondolewa vikwazo vya Marekani japokuwa bado imewekwa katika orodha ya nchi eti zinazounga mkono ugaidi. Hii ni katika hali ambayo, maafisa wa serikali ya Sudan walitarajia kwamba, kufutwa kwa vikwazo hivyo kungeboresha hali ya nchi hiyo. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, katika miaka ya hivi karibuni Sudan inasumbuliwa sana na matatizo mengi hususan katika upande wa uchumi.
Pamoja na hayo hatua ya al Bashir ya kuelekea upande wa Russia katika mazingira ya sasa inaweza kufasiriwa kuwa ni mwanzo wa kusambaratika ndoa ya Sudan na Saudi Arabia. Kabla ya safari hiyo ya Moscow, Rais al Bashir alitangaza kuwa nchi yake haikubaliani na misimo iliyodhidi ya Iran na tangazo la vita la baadhi ya nchi za Kiarabu dhidi ya Jamhuri ya Kislamu.
Rais Omar al Bashir wa Sudan alikuwa akiashiria kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kilichofanyika Jumapili iliyopita mjini Cairo nchini Misri kwa mwito wa Saudi Arabia kujadili maudhui ya Iran. Kikao hicho kilichosusiwa na nchi za Qatar, Lebanon, Iraq, Syria, Oman na Algeria kilitawaliwa na madai ya kukaririwa na yasiyo na msingi ya serikali ya Riyadh dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Sera hizo za Saudi Arabia dhidi ya Iran zinaungwa mkono na kuchochewa na Marekani na Israel.
Katika upande mwingine miongoni mwa malengo ya safari ya sasa ya al bashir nchini Russia ni kutaka kununua silaha kwa ajili ya kuimarisha jeshi la Sudan. Kwa kuzingatia kwamba, sehemu kubwa ya silaha za jeshi la Sudan zimetengenezwa Russia na kwa miaka mingi sasa silaha hizo hazijaboreshwa na kukarabatiwa, Omar al Bashir anakusudia kujikurubisha zaidi kwa Russia na kuweza kufunga mikataba ya kijeshi na kununua silaha ili kuimarisha sekta ya ulinzi ya nchi yake.
Malengo mengine ya safari hiyo ni kuwekeana mikataba ya ununuzi wa nafaka kutokana Russia na kuyaalika makampuni ya nchi hiyo kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini Sudan.
Mchambuzi wa masuala ya siasa wa Russia, Elena Voloshin anasema: "Safari ya Omar al Bashir nchini Russia ina manufaa ya kiuchumi na kistratijia kwa nchi hiyo japokuwa maslahi ya kistratijia ya Russia ndiyo yenye umuhimu zaidi katika safari hiyo." Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Rais Vladmir Putin wa Russia anafanya jitihada za kuwa na washirika na waitifaki katika maeneo yote muhimu ya kistratijia ya mabara yote duniani. Hivyo kwa kutilia maanani umuhimu wa kijeopolitiki na kistratijia wa Sudan katika bara la Afrika, safari ya al Bashir mjini Moscow inahesabiwa pia kuwa fursa nzuri ya kupanua zaidi satua na ushawishi wa Russia katika nchi nyingine za bara hilo.