Macron: Ufaransa haitokuwa ikiwaamuru tena Waafrika nini wafanye
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema yeye anatokana na kizazi cha viongozi ambao hawatokuwa wakiwaambia Waafrika nini wafanye na badala yake ataelekeza juhudi zake katika kuimarisha uhusiano wa Afrika na Ulaya.
Katika kile kinachoonekana kama msimamo wa kujipambanua na viongozi wenzake waliomtangulia, rais huyo wa Ufaransa ambaye anaitembelea Burkina Faso katika sehemu ya safari yake ya siku tatu ya kuzitembelea nchi za magharibi mwa Afrika, amesema leo katika hotuba aliyotoa mbele ya wanafunzi wa chuo kikuu katika mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou kwamba: "mimi ninatoka kwenye kizazi ambacho hakiji kuwaambia Waafrika nini la kufanya. Ninatoka kwenye kizazi ambacho ushindi wa Nelson Mandela ni moja ya kumbukumbu zake bora za kisiasa".
Macron aidha amesema: "Sitosimama pamoja na wale wanaosema bara la Afrika ni bara la migogoro na masaibu. Nitakuwa pamoja na wale wanaoamini kwamba Afrika si bara lililotoweka au linalohitaji kuokolewa".
Mbali na Burkina Faso, rais huyo wa Ufaransa anatazamiwa kuitembelea pia Ivory Coast ambako atahudhuria mkutano wa pamoja wa Ulaya na Afrika utakaofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Abidjan.../