Njama za utawala haramu wa Israel za kujipenyeza barani Afrika
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel ambaye serikali yake inafanya njama za kujipenyeza barani Afrika amesema kuwa, ana matumaini utawala huo ghasibu utafungua ubalozi mpya katika moja ya nchi za barani hilo.
Netanyahu ambaye jana alifanya safari ya siku moja nchini Kenya kushiriki katika sherehe ya kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo amesema kwamba, Tel Aviv inataka kupanua uhusiano zaidi na nchi za Kiafrika. Waziri Mkuu wa Israel amedai kwamba, anafanya kila iwezalo kupanua ushirikiano wake na nchi za Kiafrika ambazo kwa sasa hazina uhusiano na utawala huo ghasibu.
Safari ya Benjamin Netanyahu nchini Kenya imefanyika katika hali ambayo akthari ya nchi za Kiafrika zinapinga kuwa na uhusiano wa karibu na utawala huo ghasibu ambao umekuwa ukitenda jinai za kutisha kila uchao dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni balozi wa Palestina nchini Ethiopia alisema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya harakati za kutaka kupenya katika Umoja wa Afrika. Nasir Abu Jaish, balozi wa Palestina mjini Addis Ababa Ethiopia alieleza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umo mbioni kufanya juhudi za kukubaliwa kama mtazamaji katika Umoja wa Afrika AU.
Inaelezwa kuwa, kumekuwa na upinzani mkali dhidi ya hatua za utawala wa Kizayuni za kutaka kukubaliwa kama mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika. Afrika Kusini imekuwa mstari wa mbele miongoni mwa nchi zinazokabiliana na upenyaji na ushawishi wa Israel barani Afrika. Nchi nyingine ni Morocco, Algeria na Tunisia.
Nchi hizo zimekuwa zikipinga Israel kukubaliwa kama mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrtika kutokana na siasa za ukandamizaji na mauaji za utawala huo ghasibu dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.