UN yasisitiza kufanyika uchaguzi mkuu nchini Libya mwaka ujao wa 2018
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37113-un_yasisitiza_kufanyika_uchaguzi_mkuu_nchini_libya_mwaka_ujao_wa_2018
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema Walibya watafanya uchaguzi mwaka ujao wa 2018 kwa kutumia kipindi ambapo kiwango cha uingiliaji wa nchi jirani katika masuala ya nchi hiyo kitafikia kiwango cha chini zaidi.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Dec 03, 2017 03:34 UTC
  • UN yasisitiza kufanyika uchaguzi mkuu nchini Libya mwaka ujao wa 2018

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema Walibya watafanya uchaguzi mwaka ujao wa 2018 kwa kutumia kipindi ambapo kiwango cha uingiliaji wa nchi jirani katika masuala ya nchi hiyo kitafikia kiwango cha chini zaidi.

Ghassan Salamah aliyasema hayo jana katika siku ya tatu na ya mwisho ya kikao cha nchi zinazopakana na bahari ya Mediterania kilichofanyika katika mji mkuu wa Italia, Rome. Amesisitiza kuwa uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Libya umepungua, hivyo Walibya wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa ajili ya kuitisha uchaguzi.

Salamah ameongeza kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya unafanya juhudi za dhati kuhakikisha uchaguzi huo unfanyika kwa uhuru na haki.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amebainisha kuwa wadau wote wa kisiasa nchini Libya akiwemo kamanada wa jeshi la nchi hiyo Jenerali Khalifa Haftar wanaafiki kuitishwa uchaguzi huo.

Waziri Mkuu wa serikali ya Libya inayotambuliwa na UN Fayez al-Sarraj (kushoto) na Jenerali Khalifa Haftar

Hivi sasa kuna serikali mbili zinazoshikilia hatamu za madaraka nchini Libya. Moja ni serikali ya umoja wa kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambayo iko kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli, na nyengine ni serikali iliyoko mashariki mwa nchi ambayo inaungwa mkono na bunge na baadhi ya vikosi vya ulinzi vinavyoongozwa na Khalifa Haftar.

Kulinda ardhi yote ya Libya, kuendeleza mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi na magenge yanayoendesha biashara haramu ya magendo ya binadamu na kuendelea kuwepo wimbi la wahajiri haramu kutoka nchi nyengine za Kiafrika wanaopitia Libya kwa ajili ya kuvuka mpaka na kuingia barani Ulaya ni miongoni mwa matatizo yanayoitatiza nchi hiyo hivi sasa.../