Nchi za kaskazini mwa Afrika zaunga mkono pakubwa suala la Quds
Nchi na taasisi za Kiislamu za Kiafrika zimetangaza uungaji mkono wao kwa Quds Tukufu na wananchi wa Palestinan kupitia hatua mbalimbali.
Shirika la habari la Palestina limeripoti kutoka Algiers mji mkuu wa Algeria kuwa serikali ya nchi hiyo imetangaza Jumamosi ijayo kuwa siku ya kuiunga mkono Quds Tukufu kufuatia hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuutambua rasmi mji huo kama mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Trump tarehe sita mwezi huu alitangaza kuwa Washington imeutammbua rasmi mji wa Beitul Muqaddas kama mji mkuu wa utawala wa Israel na kuuhamishia ubalozi wake mjini huko kutoka Tel Aviv licha ya hatua hiyo kukabiliwa na upinzani mkubwa kieneo na kimataifa. Uamuzi huo wa Trump umekabiliwa na wimbi la malalamiko katika pembe mbalimbali duaniani khususan katika nchi za Kiislamu na Kiarabu.
Wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali nchini Misri pia wamefanya maandamano huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina na kupiga nara za kulaani uamuzi wa Rais wa Marekani dhidi ya Quds. Wanachuo hao aidha wametangaza uungaji mkono wao kwa mji huo ulioghusubiwa na kwa wananchi wa Palestina.
Wakati huo huo Ahmad al Tayyib Sheikh Mkuu wa al Azhar nchini Misri amefanya mazungumzo ya simu na Ismail Hania Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na kusisitiza kuungwa mkono Intifadha ya wananchi wa Palestina ili kuasisi serikali huru ambayo mji mkuu wake utakuwa Beitul Muqaddas. Nao maspika wa mabunge ya Kiarabu kesho Alhamisi wameitisha kikao cha dharura huko Rabat mji mkuu wa Morocco kwa lengo la kuchunguza hatua hiyo ya Trump dhidi ya Palestina.