Uganda yaalika mashirika zaidi ya Iran kuwekeza nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37681-uganda_yaalika_mashirika_zaidi_ya_iran_kuwekeza_nchini_humo
Spika wa Bunge la Uganda ametoa wito kwa mashirika ya Iran yaimarishe zaidi uwekezaji nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 16, 2017 12:00 UTC
  • Uganda yaalika mashirika zaidi ya Iran kuwekeza nchini humo

Spika wa Bunge la Uganda ametoa wito kwa mashirika ya Iran yaimarishe zaidi uwekezaji nchini humo.

Rebecca Kadaga, Spika wa Bunge la Uganda ameyasema hayo katika mkutano wake na Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kampala, Sayyid Murtadha Murtadhawi. Huku akiashiria safari ya hivi karibuni nchini Uganda ya Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kufunguliwa kituo cha tiba ambacho kilijengwa na sekta binafsi ya Iran na pia kufanyika kongamano  la kiuchumi la nchi mbili, Bi. Kadaga amesema nukta hizo zote zinaashiria upana wa uhusiano wa Tehran na Kampala.

Kituo cha Tiba cha Iran na Uganda kilifunguliwa Oktoba 26 mjini Kampala katika sherehe ambayo ilihudhuriwa na  Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran.

Spika wa Bunge la Uganda aidha amesema kuna nyuga mbalibali za kupanua uhusiano wa kiuchumi baina ya Iran na Uganda na kwa msingi huo ametoa wito kwa mashirika ya Iran yashiriki zaidi katika miradi ya maendeleo nchini Uganda hasa uwekezaji katika sekta za kilimo na ujenzi wa miundombinu ya sekta za mafuta, gesi, madini, nishati na barabara.

Rais Museveni akifungua kituo cha tiba cha Iran na Uganda mjini Kampala

Kwa upande wake, Sayyid Murtadha Muradhawi Balozi wa Iran mjini Kampala ametoa ufafanuzi kuhusu uwezo wa mashirika ya Iran na kusema tayari kuna mashirika kadhaa ya Iran nchini Uganda huku akitangaza kuwa Wairani wako tayari kuimarisha uhusiano zaidi na Uganda.

Aidha Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uganda amepongeza ushirikiano wa karibu wa Tehran na Kampala katika mashirika ya kimataifa na hasa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Vilevile amemkabidhi Bi. Kaddaga mwaliko wa Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu,Bunge la Iran, kutembelea Iran. Bi. Kadagga amepokea mwaliko huo vizuri na ameelezea matumaini yake kuwa atafika Iran katika wakati uliopangwa.