UN yairuhusu Russia kupeleka silaha Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37697-un_yairuhusu_russia_kupeleka_silaha_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Russia imepata idhini ya Umoja wa Mataifa kupeleka silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa ajili ya kutumiwa na jeshi la nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 16, 2017 22:05 UTC
  • UN yairuhusu Russia kupeleka silaha Jamhuri ya Afrika ya Kati

Russia imepata idhini ya Umoja wa Mataifa kupeleka silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa ajili ya kutumiwa na jeshi la nchi hiyo.

Idhini hiyo imetolewa kwa njia maalumu kwani Umoja wa Mataifa umeiwekea vikwazo vya silaha Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Duru zinasema Marekani, Ufaransa na Uingereza zilikuwa zimepinga idhini hiyo zikitaka kwanza kupewa maelezo kamili kuhusu silaha hizo.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitoa mwito kwa Russia miezi kadhaa iliyoipita kuipa silaha za kutumiwa na batalioni mbili mpya za kijeshi nchini humo. Russia imesema itatuma silaha ndogo ndogo kwa batalioni hizo kati ya Februari 1 na Aprili 1 mwakani na pia inajenga ghala maalumu za kuzihifadhi silaha katika nchi hiyo inayokumbwa na mapigano. Halikadhalika wakuu wa Russia wametangaza azma yao ya kutoa mafunzo ya kutumia silaha hizo kwa jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati iwapo Umoja wa Mataifa utaidhinisha suala hilo.

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati  yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya rais Muislamu, Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. 

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa mjini Bangui

Djotidia alilazimishwa na nchi za kieneo kujiuzulu mwezi Januari 2014 na hapo mauaji ya Waislamu yakashika kasi zaidi. Kabla ya kuanza mgogoro, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui, ulikuwa na wakaazi 130,000 Waislamu lakini sasa taarifa zinasema idadi hiyo ni chini ya 1,000.

Aidha watu zaidi ya 400,000, wengi wakiwa ni Waislamu wamelazimika kukimbia makazi yao huku wengine milioni 2.7, au nusu ya watu wote CAR wakiwa wanahitaji kusaidiwa. Mauaji ya Waislamu CAR yanajiri licha ya kuwepo vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini humo.