Burundi yatoa mwito wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37709-burundi_yatoa_mwito_wa_kuimarisha_uhusiano_wa_kibiashara_na_iran
Mkuu wa Jumuiya ya Biashara na Viwanda ya Burundi ametoa mwito wa kuimarishwa uhusiano wa kibiashara wa nchi hiyo ya Kiafrika na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 17, 2017 04:32 UTC
  • Burundi yatoa mwito wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Iran

Mkuu wa Jumuiya ya Biashara na Viwanda ya Burundi ametoa mwito wa kuimarishwa uhusiano wa kibiashara wa nchi hiyo ya Kiafrika na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Audace Ndayizeye ametoa wito huo katika mazungumzo yake na Murtadha Murtadhawi, balozi wa Iran huko Burundi anayeishi nchini Uganda.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Burundi amesema nchi hiyo kwa sasa inatoa kipaumbele kwa suala la kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Iran katika nyuga za kilimo, teknolojia, masuala ya uhandisi, uchimbaji madini, gesi na biadhaa za petrokemikali.

Aidha amesema nchi hiyo ingependa kustafidi na uzoefu wa Iran katika sekta za miundombinu, nishati na uzalishaji wa saruji.

Mkuu wa Jumuiya ya Biashara na Viwanda ya Burundi kadhalika amesema nchi hiyo ina uwezo wa kuiuzia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bidhaa kama chai, majani, pamba na sukari kwa bei nafuu.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi akipokea vitambulisho vya Murtadha Murtadhawi, Balozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye si mkazi, Julai mwaka huu

Kwa upande wake, Murtadha Murtadhawi, Balozi wa Iran nchini Burundi mwenye makao yake nchini Uganda amemualika Audace Ndayizeye, Mkuu wa Jumuiya ya Biashara na Viwanda ya Burundi na timu yake kuitembelea Iran ili kutizama kwa karibu na kustafidi na uwezo mkubwa wa Iran katika masuala ya viwanda na uzalishaji wa bidhaa mbali mbali.

Hali kadhalika amesisitiza kuhusu ulazima wa kutekelezwa mapatano ya nchi mbili katika uga wa kustawisha uhusiano na uwekezaji wa mashirika ya Iran nchini Burundi.