Waasi Sudan wakataa makubaliano ya amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i3784-waasi_sudan_wakataa_makubaliano_ya_amani
Makundi ya wanamgambo wenye silaha Sudan bado hayataki kukubali makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika huku serikali ya Sudan ikisisitiza makubaliano hayo ni ya mwisho na hayawezi kubadilishwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2016 11:21 UTC
  • Waasi Sudan wakataa makubaliano ya amani

Makundi ya wanamgambo wenye silaha Sudan bado hayataki kukubali makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika huku serikali ya Sudan ikisisitiza makubaliano hayo ni ya mwisho na hayawezi kubadilishwa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo ujumbe wa usuluhishi wa Umoja wa Afrika umeweka tarehe 28 mwezi huu kama siku ya mwisho kwa vyama vyote vya Sudan kusaini makubaliano ya utekelezaji wa mpango wa amani.

Serikali ya Sudan Jumatatu ilisaini kwa upande mmoja utekelezaji wa mpango huo huko Addis Ababa nchini Ethiopia, uliotolewa na ujumbe wa usuluhishi wa Umoja wa Afrika, kuhusu kusimamisha vita katika maeneo mawili ya Sudan, sehemu ya eneo la Darfur kuingia katika mchakato wa amani na kushirikisha makundi yenye silaha kwenye mazungumzo ya kitaifa yanayofanyika hivi sasa huko Khartoum.

Maeneo ya magharibi na kusini mwa Sudan yamekumbwa na hali ya mchafukoge kutokana na hujuma zinazoendeshwa na waasi na kujiri mapigano ya kikabila. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, hadi kufikia sasa watu milioni mbili na laki tano wamekuwa wakimbizi kutokana na machafuko hayo huko Sudan.

Baraza la Usalama mwaka uliopita lilipitisha azimio nambari 2228 lililoongeza muda wa walinda amani wa UN na AU nchini Sudan hadi mwezi Juni mwaka huu.