Dec 21, 2017 16:16 UTC
  • Kiongozi mpya wa chama tawala nchini Afrika Kusini aahidi kupambana na ufisadi

Cyril Ramaphosa kiongozi mpya wa chama tawala nchini Afrika Kusini ANC amesema leo kuwa ameazimia kukomesha ufisadi na kutekeleza sera ya mageuzi makali ya kiuchumi ambayo yataharakisha utaifishaji wa ardhi bila ya fidia.

Cyril Ramaphosa aliye na miaka 65 aliyekuwa mkuu wa Muungano wa Biashara wa Afrika Kusini, na kisha akawa mfanyabishara na sasa akitambulika kama mmoja wa shakhsia tajiri nchini humo kwa kiasi kikubwa anatazamiwa kuwa Rais wa baadaye wa nchi hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2019 kutokana na nguvu iliyonayo chama chake katika uchaguzi.

Kiongozi mpya wa chama tawala ANC ameahidi kupambana na ufisadi mkubwa na kufufua uchumi; ujumbe uliopongezwa na wawekezaji wa nje. Ramaphosa ameyasema hayo leo katika hotuba yake ya kwanza pambizoni mwa mkutano wa chama hicho uliodumu kwa siku tano ambako alichaguliwa kushika wadhifa huo.

Aidha ameeleza kuwa wanapaswa kuchukua hatua bila uwoga dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka katika nyadhifa wanazoshikilia. Ramaphosa ambaye ni Makamu wa Rais wa Afrika Kusini Jumatatu iliyopita alichaguliwa kuwa Kiongozi Mpya wa chama tawala ANC na hivyo kumrithi Rais Jacob Zuma kama Mwenyekiti wa chama hicho baada ya uongozi wa Zuma kukabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini  

Kiongozi mpya wa chama tawala cha ANC cha nchini Afrika Kusini pia amemshukuru Zuma katika hotuba yake hiyo akisema kuwa chama hicho kitakuwa kitu kimoja licha ya kufanyika kampeni za kimirengo wakati wa uchaguzi wa kumtafuta mwenyekiti mpya wa chama. Itakumbukwa kuwa Rais Jacob Zuma alikuwa akimuunga mkono mke wake wa zamani bi Nkosazana Dlamini  Zuma katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa chama hicho tawala.    

 

 

 

 

 

 

 

 

Tags