Jul 31, 2023 02:31 UTC
  • Woga wa Marekani wa kukumbwa huko Ukraine na yale yale yaliyoikumba Washington nchini Afghanistan

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeonya kuhusu athari mbaya za ufisadi wa kiserikali nchini Ukraine kutokana na misaada isiyo na mahesabu ya kiuchumi inayomiminiwa nchi hiyo ya Ulaya Mashariki.

Mchunguzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ametoa ripoti yake na kutahadharisha kwamba misaada ya kiuchumi ya Marekani kwa Ukraine imeiweka Washington katika hatari ya kukumbwa na ufisadi wa serikali ya Kyiv na kuna hatari pia Marekani ikakumbwa na uzoefu mchungu iliokumbana nao nchini Afghanistan.

Kabla ya hapo Wizara ya Ulinzi wa Marekani ilikuwa imekiri kuwepo ufisadi ndani ya serikali ya Ukraine lakini ilijaribu kukhafifisha suala hilo kwa kudai kuwa silaha inazopewa Kyiv zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Hii ni katika hali ambayo ripoti nyingi tu zinaonesha kuwa silaha za Marekani zinazopelekwa Ukraine zinaishia kwenye masoko ya magendo ya silaha katika kona mbalimbali ulimwenguni.

Rais kizee wa Marekani, Joe Biden

 

Hatua ya Marekani ya kutangaza rasmi kuwa ina wasiwasi wa kutumiwa vibaya misaada ya kifedha kutokana na ufisaidi uliokithiri ndani ya serikali ya Ukraine ni kukiri kusiko rasmi Washington kwamba serikali ya Kyiv ni miongoni mwa serikali zilizozama kwenye ufisadi wa kupindukia barani Ulaya. Nchi hiyo ya Ulaya Mashariki ina historia ndefu ya ufisadi na kutawaliwa na serikali legelege kiasi kwamba Shirika la Uwazi la Kimataifa limeiweka Ukraine katika nambari ya 122 ya nchi 180 zenye ubadhirifu na ufisadi mkubwa zaidi duniani. Katika ripoti hiyo, shirika hilo limesema, Ukraine ndiyo nchi yenye ufasadi mkubwa zaidi wa kifedha barani Ulaya. Hivi sasa hali ni mbaya zaidi kwani uchumi wa Ukraine umeporomoka vibaya katika miaka ya hivi karibuni. Rais wa nchi hiyo, Volodymyr Zelenskyy amekiri kuweko ufisadi wa kuchupa mipaka nchini mwake na kusema kwamba, ubadihirifu na ufisadi ni mgogoro sugu nchini Ukraine na baada ya kuanza vita na Russia, mgogoro huo umeongezeka sana na hauvumiliki kabisa.

Ubadhirifu wa mali ya uma na ufisadi wa kifedha nchini Ukraine umeongezeka mno hivi sasa kutokana na misaada mikubwa ya kifedha, kijeshi na kisilaha ya madola ya Magharibi hasa Marekani. Takwimu zinaonesha kuwa, utajiri wa viongozi wengi wa ngazi za juu wa Ukraine tangu baada ya kuanza vita na Russia umeongezeka kupindukia. Ongezeko hilo lisilo la kawaida la utajiri wa viongozi wa ngazi za juu wa Ukraine limewatia hofu viongozi wa madola ya Magharibi yanayomimina misaada yao ya kila namna nchini humo, bali hata rais wa Ukraine amelazimika kukiri kwamba ubadhirifu ni mkubwa mno na hauvumiliki. Si hayo tu lakini pia wanasiasa wa Marekani hasa wa chama cha Republican wameonesha waziwazi wasiwasi wao na wametaka kuweko usimamiaji wa kina wa fedha za Washington zinazomiminwa kwenye mifuko ya serikali ya Ukraine.

Ukraine imesambaratishwa vibaya na vita. Ndiyo nchi yenye ufisadi na ubadhirifu zaidi barani Ulaya

 

Ufisadi ndani ya serikali ya Ukraine ni mkubwa kiasi kwamba mwezi Januari mwaka huu wa 2023, rais wa nchi hiyo, Volodymyr Zelenskyy aliwafuta kazi zaidi ya maafisa 12 wa ngazi za juu wa serikali yake na siku chache baadaye alitiwa mbaroni naibu waziri wa serikali ya Kyiv kwa shutuma za ufisadi na ubadhirifu. Hatua ya rais wa Ukraine ya kuwatimua serikalini zaidi ya maafisa wake 12 kulizusha malalamiko ya wafuasi wa chama cha Republican dhidi ya Joe Biden nchini Marekani kwamba rais huyo anaipa Ukraine msaada wa makumi ya mabilioni ya dola na silaha za kila namna bila ya kuwa na uangalizi unaotakiwa wa kujua fedha na silaha hizo zinaishia wapi.

Amma nukta muhimu zaidi hapa ni kwamba, Marekani imetangaza wasiwasi wake wa kukumbwa huko Ukraine na uzoefu ule ule ulioikumbwa Washington nchini Afghanistan katika hali ambayo mwishoni mwa mwezi Agosti 2021 Marekani ililazimika kukimbia nchini Afghanistan na kudai kuwa katika kipindi chote cha miaka 20 ya kuikalia kwa mabavu Afghanistan ilitumia mabilioni ya dola katika kile ilichodai ni kuijenga upya Afghanistan lakini sasa imebainika kwamba sehemu kubwa ya fedha hizo zimepotea bure. Hivi sasa pia serikali ya Marekani imeipa Ukraine mabilioni ya dola ambazo ni fedha za walipa kodi nchini Mraekani na matokeo yake ni fedha hizo kuishia kwenye mifuko ya viongozi mafisadi na wabadhirifu wa serikali ya Kyiv na silaha zake kutumbukia kwenye magendo ya silaha katika kona mbalimbali za dunia. 

Tags