Sudan, Rwanda kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi barani Afrika
Sudan na Rwanda zimekubaliana kuunganisha juhudi zao za kutafuta suluhisho la amani la changamoto zinazolikabili bara la Afrika na kupambana na ugaidi na uhalifu wa kuchupa mpaka.
Makubaliano hayo yametangazwa kwenye taarifa ya pamoja, na yanasema pande hizo mbili zimekubaliana pia kuhimiza ushirikiano wa pande zote.
Makubaliano hayo yamefikiwa kati ya Rais Omar al Bashir wa Sudan na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame ambaye jana Alkhamisi alimaliza ziara ya siku mbili nchini Sudan.
Rais al-Bashir amesema Sudan ina urafiki wa kihistoria na wa muda mrefu na Rwanda, na amepongeza ushiriki wa Rwanda kwenye Tume ya Umoja wa Mataifa mjini Darfur.
Rais Kagame kwa upande wake amesema, Suudan na Rwanda zitazidi kuimarisha uhusiano wao kwani zinakabiliana na changamoto za pamoja. Kagame aliwasili Khartoum Jumatano kwa mwaliko wa Rais Bashir.
Katika mkutano wake na Kagame, Rais wa Sudan alizitaka nchi za Afrika kutekeleza uamuzi uliotolewa katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika na kujitoa kwenye uanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ICC kama mahakama hiyo itashindwa kujibu matakwa ya Afrika.
Rais al-Bashir amesema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Khartoum. Rais al-Bashir amesifia msimamo imara wa Rwanda katika kuunga mkono juhudi za Sudan za kutetea haki katika majukwaa ya kikanda na kimataifa pamoja na msimamo wake dhidi ya mahakama ya ICC. Pia ameisifu Rwanda kwa mchango wake mkubwa katika juhudi za kulinda amani na kuleta utulivu barani Afrika kupitia ushiriki wake katika majukumu ya ulinzi wa amani.