Mahasimu Sudan Kusini watia saini mapatano ya usitishaji vita
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37927-mahasimu_sudan_kusini_watia_saini_mapatano_ya_usitishaji_vita
Serikali ya Sudan Kusini imetiliana saini mapatano ya usitishaji vita na makundi ya waasi nchini humo jana Alkhamisi katika jitihada za hivi karibuni za kumaliza vita vya ndani ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka minne nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 22, 2017 03:18 UTC
  • Mahasimu Sudan Kusini watia saini mapatano ya usitishaji vita

Serikali ya Sudan Kusini imetiliana saini mapatano ya usitishaji vita na makundi ya waasi nchini humo jana Alkhamisi katika jitihada za hivi karibuni za kumaliza vita vya ndani ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka minne nchini humo.

Mapatano hayo yanalenga kuhuisha makubaliano ya amani ya mwaka 2015 ambayo yalivunjika mwaka jana baada ya kuibuka mapigano katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Mapatano hayo yamefikiwa katika kikao kilichoitishwa na jumuiya ya kieneo ya IGAD  mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza mwezi Disemba 2013 vimeshasababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Salva Kiir na Machar katika mapatano ya huko nyuma

Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.

Mahasimu hao wawili walituma wawakilishi katika mazungumzo hayo ya Addis Ababa. Waziri wa Habari wa Sudan Kusini Makuei Leuth amesema usitishaji vita utaanza masaa 72 baada ya jana Alkhamisi.