Umoja wa Afrika wakaribisha makubaliano ya amani ya Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37937-umoja_wa_afrika_wakaribisha_makubaliano_ya_amani_ya_sudan_kusini
Umoja wa Afrika (AU) umetoa taarifa rasmi na kukaribisha kwa mikono miwili makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya mahasimu wa kisiasa huko Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 22, 2017 11:42 UTC
  • Umoja wa Afrika wakaribisha makubaliano ya amani ya Sudan Kusini

Umoja wa Afrika (AU) umetoa taarifa rasmi na kukaribisha kwa mikono miwili makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya mahasimu wa kisiasa huko Sudan Kusini.

Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ametangaza leo kwamba, umoja huo unaunga mkono makubaliano ya amani yaliyofikiwa kati ya serikali ya Sudan Kusini na makundi ya waasi katika nchi hiyo.

Moussa Faki Mahamat amesisitiza katika taarifa yake hiyo kwamba, makubaliano hayo ni hatua ya kwanza madhubuti kwa ajili ya kuhitimisha mapigano na mauaji huko Sudan Kusini yaliyoanza Disemba mwaka 2013.

Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika

Jana serikali ya Sudan Kusini ilitiliana saini mapatano ya usitishaji vita na makundi ya waasi nchini humo ikiwa ni katika jitihada za hivi karibuni za kumaliza vita vya ndani ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka minne nchini humo.

Mapatano hayo yanalenga kuhuisha makubaliano ya amani ya mwaka 2015 ambayo yalivunjika mwaka jana baada ya kuibuka mapigano katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. Mapatano hayo yamefikiwa katika kikao kilichoitishwa na jumuiya ya kieneo ya IGAD  mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir anayetoka katika kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba, alihusika na njama za jaribio la kuipindua serikali yake.