Majaji wa Ufaransa wamlaumu Rais Kagame kuhusu mauaji ya kimbari ya Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37967-majaji_wa_ufaransa_wamlaumu_rais_kagame_kuhusu_mauaji_ya_kimbari_ya_rwanda
Majaji nchini Ufaransa wamewalaumu wapiganaji walioongozwa na Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame kwa kuilenga na kuiangusha ndege iliyokuwa imembeba Rais wa wakati huo wa taifa hilo, Juvenal Habyarimana 1994.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2017 04:04 UTC
  • Majaji wa Ufaransa wamlaumu Rais Kagame kuhusu mauaji ya kimbari ya Rwanda

Majaji nchini Ufaransa wamewalaumu wapiganaji walioongozwa na Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame kwa kuilenga na kuiangusha ndege iliyokuwa imembeba Rais wa wakati huo wa taifa hilo, Juvenal Habyarimana 1994.

Lawama za majaji hao zimetolewa baada ya kukamilika kwa uchunguzi kuhusiana na chanzo cha mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyotokea 1994. Uchunguzi huo ulikuwa ukifanywa na majaji hao wa Ufaransa juu ya shambulio la kombora lililosababisha kifo cha Rais Habyarimana na baadaye kusabisha kuanza kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka huo huo.

Uchunguzi huo uliochukua muda mrefu ndio ulikuwa chanzo cha kudorora kwa uhusiano kati ya Ufaransa na Rwanda kutokana na tuhuma kuwa, wapiganaji wa Kitutsi waliokuwa wanaongozwa na Rais wa sasa wa Rwanda Paul Kagame ndio waliohusika katika kuangusha ndege hiyo Aprili 1994.

Rais Paul Kagame wa Rwanda

Inaelezwa kuwa, kombora hilo liliitungua ndege ya Rais Habyarimana jirani na uwanja wa ndege wa Kigali na kusababisha mauaji  ya siku 100 ya Watutsi yaliyofanywa na Wahutu wa kabila la Rais Habyarimana ambapo watu zaidi ya laki 8 waliuawa. Hata hivyo Rwanda nayo inailaumu Ufaransa kwa kushiriki na kupanga mauaji hayo ya kimbari. 

Uhusiano wa nchi hizi mbili ulizidi kudorora mwezi Octoba mwaka 2016 pale majaji wa mahakama za Ufaransa walipoamua kufungua jalada upya la uchunguzi kuhusu shambulio la ndege ya Rais Habyarimana kwa kuwa timu ya raia wa Ufaransa walikuwa miongoni mwa waliokufa.