Safari ya Rais wa Ufaransa huko Niger
(last modified Sat, 23 Dec 2017 12:44:38 GMT )
Dec 23, 2017 12:44 UTC
  • Safari ya Rais wa Ufaransa huko Niger

Rais wa Ufaransa amewasili Niger kwa lengo la kukutana na wanajeshi wa nchi hiyo na kuchunguza hali ya mambo katika nchi za magharibi mwa Afrika.

Akiwa nchini Niger, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa atakutana na kufanya mazungumzo na wanajeshi wa nchi hiyo walioko katika eneo la Sahel na kuchunguza pia hali ya uthabiti huko magharibi mwa Afrika. Macron na Rais wa Niger Mahamadou Issoufou watakuwa na mazungumzo katika ikulu ya rais huyo huko Niamey. Eneo la magharibi mwa Afrika kwa muda sasa linakabiliwa na makundi ya kigaidi na migogoro ya kisiasa na kibinadamu ambayo ni natija ya ukosefu wa amani na machafuko. 

Kama anavyosema Muhammad Ibn Chambas Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko magharibi mwa Afrika: Misimamo ya kufurutu ada na ugaidi vimesababisha migogoro mingi ya kibinadamu katika eneo la Sahel barani Afrika na kuutumbukiza katika hatari kubwa umoja wa ardhi na mamlaka ya  kitaifa ya nchi za eneo hilo. 

Muhammad Ibn Chambas, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa UN magharibi mwa Afrika 
 

Viongozi wa Ufaransa wanatumia hali hii ya mambo kama kisingizio kwa ajili ya kuweko kwao kijeshi katika eneo hilo. Oparesheni kwa jina la "Barkhane" ilianza kutekelezwa katika eneo la Sahel tarehe Mosi Agosti mwaka 2014 na kuchukua nafasi ya ile iliyopewa jina la oparesheni "Serval" na hivi sasa karibu wanajeshi elfu nne wa Ufaransa wanashiriki kwenye oparesheni hiyo. 

Wanajeshi wa Ufaransa katika oparesheni nchini Niger 

Ufaransa inashiriki katika oparesheni hiyo ikiwa imetuma vikosi vyake katika nchi tano za eneo hilo ikiwemo huko Chad, Niger, Mali, Mauritania na Burkina Fasso; huku jukumu kuu la vikosi hivyo likitajwa kuwa ni kupambana na makundi yenye misimamo mikali yanayobeba silaha khususan tawi la mtandao wa kigaidi wa al Qaida katika eneo la Maghreb.

Tawi la mtandao wa kigaidi wa al Qaida katika eneo la Maghreb 

Kuendelea kwa hali hii kumetoa msukumo kwa Ufaransa si tu wa kuimarisha uwepo wa wanajeshi wake katika eneo hilo la Afrika, bali kumeipelekea nchi hiyo kuunga mkono jitihada za kuanzisha kikosi cha kijeshi cha kieneo (G-5);  na hivyo kuiwezesha Paris kuchukua uongozi wa kikosi hicho cha kijeshi huko magharibi mwa Afrika.   

Aidha suala la wahajiri na wakimbizi wanaotoka katika nchi za eneo la Sahel barani Afrika na jitihada zao za kufika katika mipaka ya nchi za Ulaya ni kadhia nyingine iliyowapelekea viongozi wa Ulaya kufanya juhudi za kulidhibiti na kulisimamia suala hilo kwa kufanya ziara huko magharibi mwa Afrika. Niger ni miongoni mwa nchi ambazo Ufaransa inafanya kila iwezalo kuwashawishi viongozi wazo kupitia kuwapatia misaada ya kifedha, wadhibiti na kuzuia wimbi la wahajiri haramu wanaoelekea barani Ulaya, kwa kuasisi vituo muhimu katika nchi hizo. Kama alivyobainisha huko nyuma Rais Macron wa Ufaransa,  Paris itafungua ofisi huko Chad na Niger ili kuwatambua wale wote wenye hali ya ukimbizi. 

Maliasili adhimu za madini ya urani na dhahabu ni sababu nyingine iliyowafanya viongozi wa Ufaransa kuwa na jicho la tamaa na hivyo kuimarisha kuweko kwao huko magharibi mwa Afrika. Niger ni miongoni mwa nchi wazalishaji wakubwa wa madini ya urani duniani. Kwa kuzingatia mgogoro wa kiuchumi uliolikumba bara Ulaya,  Ufaransa ingali inahitaji kuboresha uhusiano wake na nchi za eneo hilo ikiwemo Niger; jambo linalopewa kipaumbele na viongozi wa Ufaransa. Kiujumla tunaweza kusema kuwa ziara ya Rais Emmanuel Macron huko Niger katika kipindi hiki imefanyika kwa lengo la kuwapa moyo wanajeshi wa nchi hiyo walioko Niger na wakati huohuo kuimarisha uhusiano wa Paris na viongozi wa Niger ili kutimiza malengo ya Ufaransa nchini humo.

Tags