Wanyarwanda waishio nje kama wakimbizi warejee, ukimbizi wao utafutwa na UNHCR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37993-wanyarwanda_waishio_nje_kama_wakimbizi_warejee_ukimbizi_wao_utafutwa_na_unhcr
Rwanda imewahimiza raia wake wanaoishi kama wakimbizi katika mataifa mengine, kurejea nchini kabla ya Disemba 31, mwaka 2017 ambayo ni tarehe rasmi ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR ya kufuta ukimbizi wao.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 23, 2017 23:55 UTC
  • Wanyarwanda waishio nje kama wakimbizi warejee, ukimbizi wao utafutwa na UNHCR

Rwanda imewahimiza raia wake wanaoishi kama wakimbizi katika mataifa mengine, kurejea nchini kabla ya Disemba 31, mwaka 2017 ambayo ni tarehe rasmi ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR ya kufuta ukimbizi wao.

Zaidi ya wakimbizi 20,000 kutoka Rwanda wanatarajiwa kufutiwa hadhi yao ya ukimbizi kwa mujibu wa UNHCR.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigali, Waziri wa Rwanda anayeshughulikia Usimamizi wa Majanga na Wakimbizi Jeanne d'Arc De Bonheur, amewaonya Wanyarwanda watakaokaidi kurejea kabla ya tarehe ya mwisho kuwa watatambuliwa kama wahamiaji haramu katika mataifa wanayoishi.

Waziri huyo pia amesema, serikali ya Rwanda imewasaidia wakimbizi wa rais wa nchi hiyo kupata nyaraka muhimu, zikiwemo pasi za kusafiria kupitia balozi za Rwanda ama kwa kupitia anwani ya mtandao ya Shirika la Uhamiaji.

Mji mkuu wa Rwanda, Kigali

Takribani Wanyarwanda 84,596 wamerejeshwa makwao katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2017, ambapo asilimia 78 kati ya hao walikuwa wakiishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.