Dec 24, 2017 15:40 UTC
  • Boko Haram yaua watu watatu nchini Cameroon

Duru za kieneo zimetangaza kuwa watu wasiopungua watatu wameuawa katika shambulio la kigaidi la kundi la wakufurishaji la Boko Haram, kaskazini mwa Cameroon.

Duru hizo zimeongeza kuwa, shambulio la kwanza lilitokea Ijumaa usiku katika eneo la Mayo Moskota karibu na mpaka wa Cameroon na Nigeria wakati magaidi wa Boko Haram walipoingia kwenye mji wa Zeneme na kuua watu wawili.

Shambulizi jengine limetokea katika mji wa Kerawa-Mafa ambapo magaidi wa Boko Haram waliuvamia mji huo na kuua mtu mmoja.

Genge la kigaidi la Boko Haram linahusika katika mauaji mengi katika nchi nne za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon

 

Eneo la kaskazini mwa Cameroon ambalo linapakana na Nigeria limekuwa uwanja wa mashambulizi ya kundi la wakufurishaji la Boko Haram kwa miaka kadhaa sasa. Mashambulio hayo yameongezeka katika wakati huu wa mwishoni mwa mwaka wa 2017 Milaadia.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, magaidi wa Boko Haram walifanya mashambulizi mawili na kuua raia watatu katika eneo hilo.

Nchi nne za Cameroon, Nigeria, Chad na Niger zimeunda jeshi la pamoja la kupambana na magaidi hao lakini hadi hivi sasa zimeshindwa kuzuia mashambulizi yao.

Mashambulizi ya Boko Haram yalianza mwaka 2009 nchini Nigeria kwa madai ya kupinga elimu zinazotoka nchi za Magharibi. Mashambulio ya genge hilo yalipanua wigo wake mwaka 2015 na kuingia pia katika nchi jirani na Nigeria, yaani Niger, Cameroon na Chad.

Tags