Libya yawarejesha nyumbani wahajiri haramu 142 wa Guinea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38209-libya_yawarejesha_nyumbani_wahajiri_haramu_142_wa_guinea
Libya imewarejesha nchini kwao wahajiri haramu wapatao 142 raia wa Guinea, ikiwa ni katika jitihada za kupunguza msongamano wa wahamiaji haramu wanaozuiliwa katika vituo mbali mbali nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 28, 2017 04:23 UTC
  • Libya yawarejesha nyumbani wahajiri haramu 142 wa Guinea

Libya imewarejesha nchini kwao wahajiri haramu wapatao 142 raia wa Guinea, ikiwa ni katika jitihada za kupunguza msongamano wa wahamiaji haramu wanaozuiliwa katika vituo mbali mbali nchini humo.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, Libya imeshirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kuwarejesha kwao wahamiaji hao wa Kiafrika.

Habari zinasema kuwa, wahajiri hao wametolewa katika miji ya Zewara na Zawya, magharibi mwa nchi hadi katika mji wa Misrata, ambapo walipandishwa ndege na kupelekwa mjini Conakry.

Wahajri wa Kiafrika wanauzwa kama bidhaa nchini Libya

Wiki iliyopita, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR lilitangaza kuwa, kundi la kwanza la wahajiri waliokuwa katika jela moja nchini Libya wamehamishiwa nchini Italia.

Ripoti za UNHCR zinaonyesha kuwa, kuna wahajiri elfu 18 katika vituo na jela zilizoko chini ya usimamizi wa serikali ya Libya.

Hivi karibuni televisheni ya CNN ilirusha hewani kanda ya video inayoonesha namna wahajiri wa Kiafrika wanavyopigwa mnada sokoni na kuuzwa kama watumwa huko Libya, aghalabu yao wakiuzwa kwa dola zisizozidi 400 za Marekani.