Askari 6 wa Misri wauawa katika shambulizi la bomu eneo la Sinai
(last modified Fri, 29 Dec 2017 08:01:47 GMT )
Dec 29, 2017 08:01 UTC
  • Askari 6 wa Misri wauawa katika shambulizi la bomu eneo la Sinai

Wanajeshi sita wa Misri wameuawa katika shambulizi la bomu lililotokea jana Alkhamisi katika eneo linalokumbwa na misukosuko la Rasi ya Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, bomu la kutegwa ardhini liliripuka baada ya kukanywagwa na gari la jeshi lililokuwa likilinda doria katika mji wa Bir al-Abd, kaskazini mwa eneo la Sinai.

Msemaji wa Jeshi la Misri katika eneo hilo, Kanali Tamer el-Rifaai amethibitisha kutokea tukio hilo na kusisitiza kuwa, afisa mmoja wa ngazi za juu na wanajeshi watano ndio waliouawa katika hujuma hiyo, baada ya kuenea habari kuwa ni makamanda wawili wameuawa.

Haya yanajiri siku chache baada ya vyombo vya sheria nchini humo kuwanyonga watu 15 waliopatikana na hatia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi yaliyoua askari usalama huko kaskazini mwa Peninsula ya Sinai.

Maafisa usalama katika kituo cha upekuzi eneo la Sinai

Wapiganaji wa makundi ya kigaidi na kiwahabi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Sinai nchini Misri dhidi ya askari usalama, polisi na vituo vya ibada kama misikiti na makanisa.

Shambulizi la hivi karibuni zaidi la matakfiri hao ni lile lililofanyika mwezi uliopita katika Msikiti wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini. Zaidi ya Waislamu 300 waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala waliuawa katika shambulizi hilo.    

Tags