Kumi wauawa katika hujuma ya kigaidi dhidi ya kanisa, Cairo
Wizara ya Afya ya Misri imetangaza kuwa, watu 10 wakiwemo askari kadhaa wa usalama wameuawa katika hujuma ya watu waliokuwa na silaha iliyolenga kanisa moja katika eneo la Halwan kusini mwa jiji la Cairo.
Taarifa ya Wizara ya Afya ya Misri imesema kuwa, askari usalama wa nchi hiyo wamekabiliana na hujuma hiyo iliyolenga Kanisa la Mar Mina la Wakristo wa Kikopt na kufanikiwa kumtia nguvuni mshambuliaji mmoja baada ya kujeruhiwa. Watu wengine kumi wamejeruhiwa.
Taarifa zinasema watu wawili waliokuwa na silaha walishambulia askari usalama waliokuwa mbele ya kanisa hilo kwa kuwamiminia risasi katika jaribio la kutaka kuingia ndani ya kanisa lakini askari usalama walifanikiwa kuua mshambuliaji mmoja na mwingine ametiwa nguvuni baada ya kujeruhiwa akijaribu kutoroka.
Hujuma hiyo ya leo imefanyika licha ya serikali ya Misri kutangaza kuwa imeimarisha usalama kwa ajili ya sherehe ya Krismasi na mwaka mpya wa 2018.
Wakristo wa Kikopti husherehekea Krismasi na kuzaliwa kwa Nabii Isa Masih tarehe 7 Januari badala ya 25 Disemba.
Wakristo wa Misri kama walivyo Waislamu wa nchi hiyo, wamekuwa wakilengwa kwa mashambulizi ya makundi ya kigaidi na kiwahabi katika miaka ya hivi karibuni.
Disemba 11 mwaka jana karibu watu 30 waliuawa katika shambulizi lililofanywa na matakfiri wa kundi la Daesh mjini Cairo dhidi ya Wakristo wa Misri.