Watu 36 wafariki dunia katika ajali ya barabarani nchini Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38327-watu_36_wafariki_dunia_katika_ajali_ya_barabarani_nchini_kenya
Watu wasiopungua 36 wamefariki dunia kufuatia ajali mbaya ya barabarani baina ya lori na basi magharibi mwa Kenya katika barabara ya Nakuru-Eldoret.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 31, 2017 04:15 UTC
  • Watu 36 wafariki dunia katika ajali ya barabarani nchini Kenya

Watu wasiopungua 36 wamefariki dunia kufuatia ajali mbaya ya barabarani baina ya lori na basi magharibi mwa Kenya katika barabara ya Nakuru-Eldoret.

Kati ya waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Migaa ni watu 28 waliokuwa ndani ya basi na dereva pamoja na mbeba mzigo wa lori.

Taarifa zinasema basi lilikuwa likelekea Nairobi na lori lilikuwa likielekea upande wa Eldoret wakati ajali hiyo ilipojiri usiku wa manane majira ya saa tisa na nusu Jumapili. Taarifa zinasema watu wengine 17 wamejurhiwa vibaya katika ajali hiyo na wamekimbizwa katika hospitali za karibu.

Mkuu wa Idara ya Trafiki katika eneo la Rift Valley Zero Arome amesema basi hilo lilikuwa likiendeshwa mwendo wa kasi katika njia ya magari ya upande wa pili wakati ajali hiyo ilipojiri.

Ajali ya barabrani magharibi mwa Kenya eneo la Migaa Dec.31 2017

Watu karibu 200 wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa katika ajali za barabarani mwezi huu wa Disemba nchini Kenya.

Akihutubia taifa wakati wa sherehe za Siku ya Jamhuri, Rais Uhuru Kenyatta aliwataka Wakenya wawe waangalifu huku akisema serikali itachukua hatua za usalama kuzuia ajali barabarani.