Ethiopia kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa
Katika hatua ya kushtukiza, Waziri Mkuu wa Ethiopia ametangaza mpango wa serikali wa kufuta mashitaka dhidi ya wafungwa wote wa kisiasa sambamba na kufunga jela ya kuogofya ambako wafungwa hao walikuwa wanazuiliwa.
Tangazo hilo la Hailemariam Desalegn Jumatano hii limekuja baada ya wimbi la maandamano dhidi ya serikali kushuhudiwa katika maeneo ya Amhara na Oromia katika miezi ya hivi karibuni.
Ghasia zilizotokana na maandamano hayo zimelemaza biashara nyingi, kuvuruga mfumo wa usafiri na kupelekea vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu kufungwa.
Desalegn amesema: "Wafungwa wa kisiasa wanaoakabiliwa na mashitaka na ambao tayari wanatumikia vifungo wataachiwa huru. Aidha gereza la kutisha la Maekelawi litafungwa na kugeuzwa kuwa makavazi."

Wapinzani na watetezi wa haki za binadamu nchini humo kwa muda mrefu wamekuwa wakishinikiza kuachiwa huru wafungwa wote wa kisiasa, wakiwemo viongozi wa upinzani, wakosoaji wa serikali na hata waandishi wa habari wanaoonekana kuikosoa serikali ya Addis Ababa.
Mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliomalizika wa 2017, watu 245 walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na machafuko ya eneo la Oromia na kuchoma moto maeneo tofauti ya jimbo hilo na vile vile kusababisha idadi kubwa ya wakazi wake kuwa wakimbizi.