AU kuchunguza mateso ya wahajiri wa Kisudan Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39383-au_kuchunguza_mateso_ya_wahajiri_wa_kisudan_libya
Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kijamii ya Umoja wa Afrika amesema kuwa, umoja huo utaanzisha uchunguzi kuhusu mateso waliyofanyiwa wahajiri wa Kisudani nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2018 11:35 UTC
  • AU kuchunguza mateso ya wahajiri wa Kisudan Libya

Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kijamii ya Umoja wa Afrika amesema kuwa, umoja huo utaanzisha uchunguzi kuhusu mateso waliyofanyiwa wahajiri wa Kisudani nchini Libya.

Amira Al Fadel amesema kuwa, AU itafanya uchunguzi kuhusu filamu mpya inayohusiana na kuteswa raia wa Sudan walioko Libya. 

Baada ya kusambaa filamu hiyo ya video inayowaonesha raia wa Sudan wakipewa mateso nchini Libya, serikali ya mwafaka wa kitaifa ya nchi hiyo imetoa taarifa ikiahidi kuwafuatilia na kuwafikisha mahakamani watu waliohusika na ukatili huo. 

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya imesema kuwa: Serikali inalaani ukatili unaofanywa dhidi ya wahajiri nchini humo. Taarifa hiyo pia imezitaka idara za masuala ya usalama na mahakama kufanya uchunguzi kuhusu uhalifu uliofanyika na kuwafikisha wahusika mahakamani. 

Wahajiri wa Kiafrika nchini Libya

Libya ndio njia kuu ya wajahajiri wanaofanya jitihada za kuelekea Ulaya ambao wengi miongoni mwao hutumbukia katika mtego wa utumwa au kughariki katika bahari ya Mediterania. 

Hivi karibuni vyombo vya habari duniani vilirusha hewani kanda ya video iliyoonesha namna wahajiri wa Kiafrika wanavyopigwa mnada sokoni na kuuzwa kama watumwa huko Libya, aghalabu yao wakiuzwa kwa dola zisizozidi 400 za Marekani.