AU: Afrika haiwezi kunyamazia kimya matusi ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39493-au_afrika_haiwezi_kunyamazia_kimya_matusi_ya_trump
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema bara la Afrika lilishtushwa na lingali linaendelea kutafakari kuhusu kauli chafu na ya kebehi iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani, kwamba wahamiaji wanaoingia nchini Marekani kutoka bara hilo, Haiti na El Salvador wanatoka kwenye nchi za "shimo la kinyesi".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2018 03:44 UTC
  • AU: Afrika haiwezi kunyamazia kimya matusi ya Trump

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema bara la Afrika lilishtushwa na lingali linaendelea kutafakari kuhusu kauli chafu na ya kebehi iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani, kwamba wahamiaji wanaoingia nchini Marekani kutoka bara hilo, Haiti na El Salvador wanatoka kwenye nchi za "shimo la kinyesi".

Dakta Moussa Faki Mahmat aliyasema hayo jana Alkhamisi katika ufunguzi wa duru ya 27 ya mkutano wa ngazi ya uwaziri wa AU, katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Amesema matamshi hayo ya kukera na yaliyojaa chuki, kebehi na yanayopigia debe suala la kuendelea kutengwa bara Afrika yaliyotolewa na Trump yalizishtua nchi za bara hilo na kusisitiza kuwa bara hilo katu haliwezi kuifumbia macho kadhia hiyo. 

Mkuu huyo wa Kamisheni wa Umoja wa Afrika amebainisha kuwa, kauli hiyo ya kejeli ya Trump, uamuzi wa Marekani dhidi ya Jerusalem (Quds Tukufu) sambamba na kupunguza bajeti yake kwa vikosi vya kimataifa vya kulinda amani ni ithibati kuwa ushirikiano wa nchi mbali mbali duniani kwa shabaha ya kufikia malengo fulani upo mashakani.

Baada ya kushutumiwa vikali, Trump alikanusha kutamka maneno hayo dhidi ya Afrika, Haiti na El Salvador

Nchi kadhaa za Afrika zimelaani kauli chafu iliyotolewa na Donald Trump kuhusiana na nchi za bara hilo huku baadhi yao zikichukua hatua ya kuwaita mabalozi wa Marekani katika nchi hizo na kuwakabidhi malalamiko yao kutokana na kejeli hizo za Trump.

Kadhalika mabalozi wanaowakilisha nchi za Afrika katika Umoja wa Mataifa wamependekeza Rais Donald Trump wa Marekani akutane na kuzungumza moja kwa moja na viongozi wa Afrika wakati viongozi hao watakapokutana mjini Addis Ababa nchini Ethiopia katika mkutano wa AU, unaotazamiwa kufanyika tarehe 28 na 29 mwezi huu.