Niger yapinga kutumwa wanajeshi wa Italia nchini humo
(last modified Sat, 27 Jan 2018 12:52:34 GMT )
Jan 27, 2018 12:52 UTC
  • Niger yapinga kutumwa wanajeshi wa Italia nchini humo

Katika hali ambayo Italia imetangaza habari ya kutumwa vikosi vyake vya kijeshi huko Niger kufuatia ombi la serikali ya Niamey, viongozi wa nchi hiyo ya Kiafrika wametangaza kuwa wanapinga kuweko wanajeshi wa Italia katika ardhi ya nchi hiyo na kwamba hawajawahi kuzungumzia suala hilo na wenzao wa Roma.

Viongozi wa Niger wamesema kuwa serikali ya nchi hiyo imeitaarifu Roma kuhusu kupinga suala hilo kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger. Kwa muda sasa viongozi wa Italia wamekuwa wakifuatilia suala la kutuma wanajeshi hiyo huko Niger. Ni wazi kuwa nchi hiyo ya Ulaya kama zilivyo baadhi ya nchi waitifaki wake kama Ufaransa, inataka kuwa na wanajeshi wake huko Niger na katika nchi nyingine za Kiafrika. 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa Italia inafanya jitihada za kuwa na nafasi na ushawishi zaidi barani Afrika. Kuhusiana na suala hilo, Angelino Alfano Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesema: Nchi za kusini mwa jangwa kubwa la Sahara barani Afrika zinahesabiwa kuwa moja ya vipaumbele vya Italia katika mwaka huu wa 2018. 

Angelino Alfano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia 

Hata kama nchi za Magharibi zimekuwepo kijeshi kwa muda mrefu barani Afrika lakini katika miaka ya karibuni nchi hizo zimekuwa zikifanya kila ziwezalo kujiimarisha zaidi kijeshi barani humo kwa kuzingatia matukio ya kisiasa na kiuchumi yaliyojitokeza kieneo na kimataifa. Nchi hizo zimekuwa zikifuatilia malengo tofauti kufuatia kuweko kwao huko kijeshi ambapo miongoni mwake tunaweza kuashiria ushindani mkubwa wa kiuchumi na kisiasa baina ya madola makubwa ya Ulaya na Marekani barani humo. 

Hata hivyo suala lililo na umuhimu hivi sasa ni kadhia ya wahajiri wa Kiafrika na vile vile kuongeza harakati za magenge ya magendo ya binadamu. Italia hivi sasa inaheabiwa kuwa lango la kuingilia wahajiri hao wanaoelekea Ulaya kufuatia kufungwa njia ya Uturuki kuelekea Ugiriki. Kwa msingi huo, nchi hiyo inatekeleza siasa za kuzuia kuingia barani Ulaya wahajiri na wahamiaji kuliko nchi nyingine yoyote ya bara hilo. Katika uga huo Niger ni moja ya nchi muhimu zaidi zinazoweza kutumiwa na wahajiri wa Kiafrika kama lango la kufika Libya na kisha kuvuka bahari ya Mediterania kuingia Italia; na kwa msingi huo moja ya sababu kuu za Italia kutaka kutuma jeshi lake huko Niger ni kutaka kudhibiti wimbi la wahajiri na kuwazuia kuondoka nchini humo kwa nia ya kuelekea Ulaya.  

Wakimbizi kutoka nchi mbalimbali za Kiafrika wakiwa safarini kuelekea Ulaya 

Wakati huo huo mapambano dhidi ya ugaidi ni kisingizio kingine kinachotumiwa na nchi za Magharibi ili kuzidisha kuwepo kwao kijeshi barani Afrika. Wanajeshi wa nchi mbalimbali za Magharibi khususan Ufaransa wapo katika nchi za Kiafrika ikiwemo Niger kwa kisingizio cha kuendesha mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi na yale yenye misimamo mikali; na hivi sasa pia Italia inataka kuwaondoa wanajeshi wake huko Iraq na kuwatuma  Afrika khususan katika nchi ya Niger. Paolo Gentiloni Waziri Mkuu wa Italia amesema kuhusu suala hilo kwamba: Italia itatuma huko Niger wanajeshi wake walioko Iraq. 

Nchi za Magharibi zinaendeleza siasa zao hizo za kujiimarisha kijeshi Afrika huku viongozi wengi wa bara hilo wakiamini kuwa  matatizo mengi ya nchi za Kiafrika chanzo chake ni uingiliaji wa nchi za Magharibi. Viongozi hao wanafanya jitihada ili kuzuia kuweko kijeshi nchi hizo barani Afrika. Kutekeleza jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kieneo kwa ajili ya kuendesha vita dhidi ya ugaidi, kutekeleza juhudi za kuimarisha miundo mbinu na kuboresha hali ya maisha ili kuzuia wimbi la wahajiri ni baadhi ya siasa zinazotekelezwa na viongozi hao katika uwanja huo. 

Tags