Misri yapokea vyema kuboreka uhusiano wa Ethiopia na Sudan
(last modified Mon, 29 Jan 2018 15:13:43 GMT )
Jan 29, 2018 15:13 UTC
  • Misri yapokea vyema kuboreka uhusiano wa Ethiopia na Sudan

Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amesema nchi yake imefurahishwa na kuboreka uhusiano baina ya Sudan na Ethiopia katika nyuga tofauti.

Amesema hayo leo pambizoni mwa kikao cha pamoja cha Rais Omar al Bashir wa Sudan na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn yaliyofanyika kwa lengo ka kutatua mizozo baina ya nchi hizo tatu. 

Rais wa Misri ameongeza kuwa, hata katika kadhia ya bwawa la al Nahdha linalojengwa na Ethiopia, hakuna mgogoro baina ya nchi hizo tatu bali jambo hilo linafanyika kwa maelewano ya pande hizo zote.

Ujenzi wa Bwawa la al Nahdha nchini Ethiopia

 

Suala la bwawa la al Nahdha ndiyo iliyokuwa ajenda kuu ya mazungumzo baina ya wakuu wa nchi za Misri, Ethiopia na Sudan, pambizoni mwa kikao cha viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Addiss Ababa.

Misri ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele kupinga mradi wa Ethiopia wa kujenga bwawa la al Nahdha ambalo litatumia maji ya Mto Nile katika miradi yake ya maendeleo. Cairo ilikuwa inapinga mradi huo kwa kuhofia kuwa utapunguza maji ya Mto Nile yanayomiminika Misri na kusababisha ukame na upungufu wa maji ya kunywa nchini humo.

Mgogoro ulizidi kuwa mkubwa baada ya Misri kuituhumu Sudan kuwa inaiunga mkono Ethiopia katika mradi wake huo.

Kwa upande wake, Ethiopia imesema ni haki yake kutumia rasilimali zake yakiwemo maji ya Mto Nile kujiletea maendeleo na kwamba upinzani wa Misri kwa jambo hilo ni kitu cha kushangaza na ni uingiliaji wa masuala ya ndani ya Ethiopia.

Tags