Wasiwasi watanda Kenya huku Odinga akijiandaa kuapishwa kama 'rais'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39675-wasiwasi_watanda_kenya_huku_odinga_akijiandaa_kuapishwa_kama_'rais'
Wasiwasi umetanda nchini Kenya hii leo katika siku ambayo Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA Raila Odinga ametangaza kuwa ataapishwa kama 'rais' hatua ambayo serikali imesema ni uhaini na hukumu yake ni kunyongwa.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jan 30, 2018 04:38 UTC
  • Wasiwasi watanda Kenya huku Odinga akijiandaa kuapishwa kama 'rais'

Wasiwasi umetanda nchini Kenya hii leo katika siku ambayo Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA Raila Odinga ametangaza kuwa ataapishwa kama 'rais' hatua ambayo serikali imesema ni uhaini na hukumu yake ni kunyongwa.

Tokea jana usiku, maafisa wa polisi wamekuwa wakilinda doria katika  uwanja wa Uhuru Park mjini Nairobi sehemu ambayo Odinga anapanga kuapishwa akiwa na naibu wake Kalonzo Musyoka. Taarifa zaidi zinasema maafisa wa polisi sasa wameondoka katika eneo hilo ili kuzuia makabiliano na wafuasi wa NASA. Aidha maafisa wa polisi wamezuia mabasi kadhaa ya wafuasi wa Nasa waliokuwa wakielekea Nairobi kutoka Mombasa kuhudhuria sherehe hizo. Tarifa zinasema televisheni za Kenya zimezuiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mjumuiko huo wa NASA katika uwanja wa Uhuru Park.

Mwanasheria Mkuu nchini Kenya Githu Muigai ameonya kuwa hatua ya kumuapisha Odinga kama rais ni ya uhaini. Muigai amesema iwapo NASA itaendelea na mipango hiyo itakua inakiuka katiba na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi wa muungano huo wa upinzani. Muigai ameonya kuwa iwapo Odinga ataapishwa hii leo, atafunguliwa mashtaka ya uhaini.

Raila Odinga (kushoto) na Rais Uhuru Kenyatta

Odinga anasisitiza kuwa alishinda uchaguzi uliofanyika Agosti nane mwaka uliopita, uchaguzi ambao ulibatilishwa na mahakama iliyaomuru uchaguzi wa marudio ufanyike. Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alitangazwa mshindi katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 26 ambao Odinga aliusisia.