Wanasiasa Misri kususia uchaguzi wa rais
(last modified Tue, 30 Jan 2018 16:36:55 GMT )
Jan 30, 2018 16:36 UTC
  • Wanasiasa Misri kususia uchaguzi wa rais

Makumi ya wanaharakati wa kisiasa wa Misri wametia saini taarifa ya kususia uchaguzi ujao wa rais nchini humo wakisema kuwa, hautakuwa na sifa za awali kabisa za uchaguzi huru na wa haki.

Taarifa hiyo pia imetaka kusitishwa kazi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuvunjwa Baraza la Uchaguzi la Misri kutokana na kukingai kifua uingiliaji wa taasisi za usalama katika uchaguzi ujao wa rais. 

Taarifa na wanaharakati wa kisiasa wa Misri pia imewataka wananchi kususia kikamilifu uchaguzi huo na kutotambua rasmi matokeo yake. 

Imesema uchaguzi huo ni mwavuli utakaotumiwa na Rais Abel Fattah al Sisi kwa ajili ya kubadili katiba ya nchi na kurefusha kipindi cha utawala wake na kuondoa fursa ya kukabidhiwa madaraka kwa njia za kidemokrasia. 

Sami Hafez Anan anashikiliwa jela baada ya kutangaza kuwa atagombea dhidi ya al Sisi

Wanaharakati wa Misri wamesisitiza katika taarifa hiyo kwamba, uchaguzi wa rais ujao wa Misri utafungua uwanja wa kudumishwa siasa za miaka iliyopita ikiwa ni pamoja na kugawa ardhi za nchi hiyo kwa nchi ajinabi, kuzidisha umaskini na kukandamiza zaidi demokrasia. 

Uchaguzi wa rais wa Misri umepangwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu na kuna uwezekano mkubwa Abdel Fattah al Sisi akawa mgombea wa pekee katika uchaguzi huo baada ya wapinzani wake ama kukamatwa, kuzuiwa au kujiengua kutokana na mazingira yasiyofaa.    

Tags