Makumi ya miili ya wahajiri yapatikana katika pwani ya Morocco
Serikali ya Uhispania imetangaza habari ya kupatikana kwa makumi ya maiti za wahajiri katika maji ya pwani ya Morocco.
Irene Flores, Mkuu wa Mawasiliano wa Serikali ya Eneo la Melilla ameliambia shirika la habari la Associated Press leo Jumapili kuwa, maafisa wa Gadi ya Pwani ya Uhispania walizipata maiti za wahajiri hao jana Jumamosi walipokuwa wakipiga doria.
Vyombo vya habari vya Uhispania vimeripoti kuwa, maiti zaidi ya 20 zimepatika katika operesheni hiyo na kwamba aghalabu ya wahajiri hao waliokuwa wakielekea Uhispania walikuwa Waafrika kutoka nchi za eneo la chini ya jangwa la Sahara.
Kila mwaka maelfu ya wahajiri hususan wa Kiafrika hufa maji katika safari hizo za kutisha za kuelekea Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean, kwenda kutafatuta maisha mazuri.
Katika hatua nyingine, meli ya mafuta iliyokuwa na mabaharia 22 raia wa India imetoweka katika pwani ya Magharibi mwa Afrika.
Raveesh Kumar, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India amesema balozi za nchi hiyo katika nchi za Nigeria na Benin zinashirikiana na serikali za nchi hizo za magharibi mwa Afrika katika jitihada za kuitafuta meli hiyo, iliyokuwa imebeba petroli tani 13,500.
Pwani za magharibi na mashariki mwa Afrika zimekuwa zikikabiliwa na mashambulizi ya maharamia kwa miaka mingi sasa.