Feb 07, 2018 02:35 UTC
  • Hotuba ya Rais Zuma katika Bunge la Afrika Kusini yaakhirishwa

Spika wa Bunge la Afrika Kusini Baleka Mbete amesema hotuba ya kila mwaka ya rais kuhusu hali ya nchi, imeakhirishwa kutokana na mashinikizo anayokabiliana nayo Rais Jacob Zuma.

Hotuba hiyo ilikuwa isomwe na Zuma Alhamisi bungeni lakini sasa imeakhirishwa hadi wakati mwingine huku rais huyo akiendelea kushinikizwa ajiuluzu.

Hayo yanajiri wakati ambao afisa mmoja wa ngazi ya juu katika chama tawala nchini Afrika Kusini (ANC) amesema kuwa Zuma anapasa kujiuzulu na hivyo kuzidisha mashinikizo dhidi ya rais huyo ambaye anaonekana kudhoofika kisiasa tangu Cyril Ramaphosa achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa chama tawala ANC mwezi Disemba mwaka jana.

Cyril Ramaphosa

Mweka hazina mkuu wa chama cha ANC Paul Mashatile ameeleza kuwa kunapasa kuwepo mabadiliko ya usimamizi na kwamba haiwezekani chama hicho kikawa na vituo viwili vya madaraka. Amesema njia bora zaidi ya kufanikisha suala hilo ni kwa rais kuondoka madarakani.

Zuma ambaye anakabiliwa na tuhuma za ufisadi amekuwa katika nafasi inayolegalega tangu nafasi yake ya mkuu wa chama tawala ANC ichukuliwe na Makamu wa Rais, Cyril Ramaphosa.

Tags