Kamanda wa Libya anayesakwa na ICC ajisalimisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40043-kamanda_wa_libya_anayesakwa_na_icc_ajisalimisha
Mahmoud Mustafa Busayf Al-Werfalli, kamanda wa ngazi ya juu huko Libya anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita amejisalimisha kwa wapiganaji watiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar mjini Benghazi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2018 11:23 UTC
  • Kamanda wa Libya anayesakwa na ICC ajisalimisha

Mahmoud Mustafa Busayf Al-Werfalli, kamanda wa ngazi ya juu huko Libya anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa tuhuma za kuhusika na jinai za kivita amejisalimisha kwa wapiganaji watiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar mjini Benghazi.

Katika video iliyosambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, kamanda huyo amesikika akisema, "Ninajisalimisha kwa jeshi  linaloongozwa na Kamanda Haftar, ambalo askari wake wanashikilia sehemu kubwa ya mashariki mwa nchi."

Kwenye video hiyo, Busayf Al-Werfalli anasisitiza kuwa hana hatia, huku akihalalisha mauaji dhidi ya magenge ya wapiganaji. 

Al-Werfalli ambaye alizaliwa mwaka 1978 ni kamanda wa ngazi ya juu katika brigedi ya al-Saiqa iliyojitenga na Jeshi la Taifa la Libya baada ya kuibuka mapambano ya kumng'oa madarakani dikteta wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mwaka 2011. 

Jenerali Khalifa Haftar 

Brigedi hiyo imekuwa ikipigana bega kwa bega na wapiganaji watiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar huko Benghazi; mji wa pili kwa ukubwa wa Libya ambao ulikombolewa hivi karibuni baada ya mapigano ya miaka mitatu.

Majaji wa Mahakama ya ICC mwezi Agosti mwaka jana walitoa waranti wa kutiwa mbaroni Al-Werfalli wakidai kuwa amehusika na mauaji ya watu 33 katika mji huo kati ya mwaka 2016 na mwaka jana.