Ikhwani yakanusha kufanya mazungumzo na serikali ya el Sisi, Misri
Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri imekanusha madai kwamba, viongozi wake wamefanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na harakati ya Ikhwanul Muslimin imesema kuwa inakadhibisha habari yoyote ya kuwepo mazungumzo, mawasiliano au muamala wa aina yoyote baina ya harakati hiyo na serikali ya Misri.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, lengo la kusambazwa madai na uvumi huo ni kuwapotosha Wamisri kuhusu maafa yaliyofanywa na utawala uliotwaa madaraka ya nchi kwa njia ya mapinduzi.
Taarifa hiyo ya harakati ya Ikhwanul Muslimin imesema kuwa, kwa mujibu wa misingi ya demokrasia na maamuzi ya wananchi, inamtambua Muhammad Morsi aliyeondolewa madarakani na Jenerali Abdel Fattah el Sisi, kuwa ndiye rais halali wa Misri na kwamba wanachama wa harakati hiyo hawawezi kusaliti misingi, maadili na matakwa yake ya kiadilifu.
Hivi karibuni gazeti la Kimarekani la Bloomberg lilidai kuwa, kuna habari kwamba serikali ya Misri inafanya mawasiliano na mazungumzo na viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin wanaoshikiliwa katika korokoro za nchi hiyo.
Kundi la Ikwanul Muslimin ambalo ndiyo chama kikubwa zaidi cha kisiasa cha upinzani nchini Misri lilipigwa marufuku na kuzuiwa kuendesha shughuli zote za kisiasa baada ya jeshi la nchi hiyo kumpindua rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia wa Misri, Muhammad Morsi mwaka 2013. Viongozi wengi wa harakati hiyo akiwemo Morsi mwenyewe, wanashikiliwa katika jela za Misri.