Mapigano yasababisha maelfu kukimbia makazi yao CAR
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC imesema maelfu ya watu wamelazimika kukimbia na kuacha makazi yao, kutoka na kushtadi mapigano kati ya makundi hasimu ya waasi huko kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Jean-Francois Sangsue, mkuu wa ICRC mjini Bangui amesema zaidi ya wakazi 7,400 wa eneo hilo wamefurushwa makwao tangu mapigano hayo yaanze mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana.
Amesema aghalabu ya watu hao wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani katika eneo la Markounda, ambapo wanapitia hali ngumu ya maisha.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema raia hao wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sasa wanaishi kwenye mahema na nyumba za muda zilizojengwa kwa mifuko ya plastiki, huku wakikosa suhula za msingi kama vyoo na bafu.
Kwa zaidi ya miezi miwili sasa, makundi hasimu ya wabeba silaha ya National Movement for the Liberation of the Central African Republic (MNLC) na Revolution and Justice (RJ) yamekuwa yakikabiliana kwa ajili ya kudhibiti eneo hilo la kaskazini magharibi mwa nchi.
Jamhuri ya Afrika ya Kati, moja ya nchi maskini zaidi duniani, imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2013; magenge ya waasi yakipigana yenyewe kwa wenye kwa upande mmoja, na vikosi vya usalama vikikabiliana na makundi hayo kwa upande mwingine.