Jeshi la Misri lawaangamiza magaidi 16 katika eneo la Sinai
(last modified Sun, 11 Feb 2018 15:44:22 GMT )
Feb 11, 2018 15:44 UTC
  • Jeshi la Misri lawaangamiza magaidi 16 katika eneo la Sinai

Jeshi la Misri limetangaza kuwa, limewaua magaidi 16 kufuatia operesheni ya kijeshi katika eneo la Sinai.

Taarifa ya jeshi la Misri iliyotolewa leo imesema kuwa, washukiwa wengine 30 wametiwa mbaroni katika operesheni hiyo ya kijeshi iliyoanza kutekelezwa katika eneo la Sinai tangu siku ya Ijumaa kwa amri ya Rais Abdul-Fattah al-Sisi wa nchi hiyo.

Jeshi la Misri limetoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi kwa ajili ya kuwaangamiza magaidi ambao wamekuwa wakihatarisha usalama katika eneo la Sinai.

Aidha taarifa ya jeshi la Misri imeeleza kuwa, vikosi hivyo pamoja na vile vya polisi vimejiweka katika hali ya tahadhari kwa ajili ya kutekeleza operesheni hiyo.

Wapiganaji wa makundi ya kigaidi wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika eneo la Sinai nchini Misri dhidi ya askari usalama, polisi na vituo vya ibada kama misikiti na makanisa.

Mlipuko katika msikiti mmoja huko Sinai Misri

Shambulio la hivi karibuni zaidi la magaidi hao ni lile la mwezi Novemba mwaka jana katika Msikiti wa al-Rawdhah ulioko katika mji wa Bir al-Abd, yapata kilomita 40 kutoka mji wa Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini. Zaidi ya Waislamu 300 waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala waliuawa katika shambulio hilo.    

Nchi ya Misri imekuwa ikishuhudia ukosefu wa amani na usalama tangu mwaka 2013 kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abdul-Fattah al-Sisi na kumuondoa madarakani Rais Muhammad Mursi aliyechaguliwa kwa njia ya demokrasia.

Tags