UN: Maelfu ya Wasudani Kusini watakimbilia Sudan mwaka huu wa 2018
Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema katika ripoti yake mpya kwamba karibu wakimbizi laki mbili kutoka Sudan Kusini wataingia nchi jirani ya Sudan mwaka huu wa 2018.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana Ijumaa imesema kuwa, mwaka huu wa 2018 karibu wakimbizi wapya laki mbili raia wa Sudan Kusini wataingia Sudan wakikimbia mapigano na njaa.
Ripoti hiyo imesema, mapigano yanayoendelea, uhaba wa misaada ya kibinadamu na njaa vitawalazimisha watu wa Sudan Kusini kukimbilia katika nchi jirani kwa ajili ya kupata huduma muhimu.
Ofisi ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa, tangu mwanzoni mwa vita vya ndani nchini Sudan Kusini mwaka 2013, raia laki nne na 17 elfu wa nchi hiyo wamekimbilia nchi jirani ya Sudan.
Sudan inatekeleza siasa za "mpaka wazi" na kuwaruhusu wakimbizi wa Sudan Kusini kuingia nchini humo bila ya kizuizi wala masharti yoyote.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011.