Ethiopia yaakhirisha mkutano wake na Misri kuhusu bwawa la al-Nahdha
Misri imekubali ombi la Ethiopia la kuakhirisha mkutano wa pande mbili wa kujadili suala tata la bwawa la al-Nahdha linalojengwa na Uhabeshi, baada ya Adiss Ababa kutangaza sheria ya hali ya hatari.
Ethiopia imetangaza hali ya hatari kwa muda wa miezi sita kufuatia kujiuzulu ghafla Waziri Mkuu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, Hailemariam Desalign.
Mkutano kuhusu mgogoro wa bwawa la al-Nahdha ulikuwa umepangwa kufanyika kati ya Februari 24 na 25 mjini Khartoum, Sudan.
Ahmed Abu Zeid, Waziri wa Mambo ya Nje ya Misri amesema Cairo 'inaelewa' sababu zilizopelekea Addis Ababa kutaka kuakhirishwa mkutano huo, na kwamba wanataraji utapangwa upya karibuni hivi.
Misri imekuwa ikipinga mradi wa Ethiopia wa kujenga bwawa la al-Nahdha ambalo litatumia maji ya Mto Nile katika miradi yake ya maendeleo, ikihofia kuwa utapunguza maji ya huo na kusababisha ukame na upungufu wa maji ya kunywa nchini humo.
Mgogoro huo ulishtadi baada ya Misri kuituhumu Sudan kuwa inaiunga mkono Ethiopia katika mradi wake huo.